Nuru FM

Bodi Ya Sukari Yaanza Mkakati Wa Kuongeza Uzalishaji

25 October 2022, 4:05 pm

BODI ya Sukari Tanzania imeanza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa sukari nchini ili kukabili na uhaba wa bidhaa hiyo ambapo wanatarajia ifikapo mwaka 2025/2026 uzalishaji wa sukari utaongezeka hadi kufikia tani laki 756.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 25,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof. Kenneth Bengesi, wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Prof. Bengesi amesema kutokana na hali nchi itakuwa na kiasi cha kutosha cha bidhaa hiyo ambayo itatosheleza mahitaji ya ndani pamoja na kuuza nje ya nchi.

“Hivi sasa uzalishaji wa sukari nchini ni tani 380,000 na mahitaji ni tani 440,000 hivyo pengo ni tani 60,000 Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatutaka hadi ifikapo 2025 kuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki 756 za sukari hivyo sisi tutakua tumevuka lengo hilo kwa kuzalisha tani 756”amesema Prof. Bengesi

MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof. Kenneth Bengesi,akizungumza na waandishi wa habari

Alisema, hivi sasa viwanda vyote vinavyozalisha sukari nchini wanafanya upanuzi ili kuongeza uzalishaji kutoka kiasi ambacho kinazalishwa sasa.

“Viwanda vyetu vyote hivi sasa tunavifanyia upanuzi ili kuongeza uzalishaji lakini kuna kiwanda kipya cha Bagamoyo Sugar ambacho tayari kimeanza uzalishaji mwaka huu.

“Mwakani pia tutaongeza uzalishaji kwa kiwanda kipya cha Mkulazi mkoani Mororogoro na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo hivi sasa kwenye mashamba ya miwa makubwa na madogo iliyopo ili kuzalisha miwa mingi na yenye ubora”amesema

Pia, amesema serikali ipo katika mipango ya kuanza uzalishaji wa sukari kwa ajili ya matumizi ya viwanda ambayo hivi sasa inayotumika nchini inaagizwa kutoka nje.

“Hatujawahi kuzalisha sukari kwa ajili ya matumizi ya viwanda hivyo inayotumika hivi sasa kiasi cha tani 205,000 yote inatoka nje hivyo kufanya serikali kutumia Dola milioni 150 sawa na zaidi ya Sh. bilioni 300 kuagiza sukari ya matumizi ya nyumbani na hii kwa ajili ya viwanda.

“Kitendo hichi cha kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza sukari nje ya nchi ni sawa na kuimarisha viwanda vya wenzako na ni aibu kuagiza sukari nje ya nchi”amesema

Katika hatua nyingine Prof. Bangesi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia suluhu Hassan imedhamiria kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kwa kujenga viwanda vingi ili kuongeza ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Zamaradi Kawawa ameipongeza bodi hiyo kwa kuwahakikishia watanzania uwepo wa sukari ya kutosha katika kipindi cha miaka miwili  na nusu ijayo.

Bodi ya Sukari Tanzania ina majukumu la kiudhibiti lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa soko na uzalishaji wa miwa inayoenda kuzalisha sukari inakuwa katika ubora unaostahili na kuendeleza na kusimamia tasnia ya sukari.