Nuru FM

Wananchi 112,669 Iringa Wamepata Chanjo Ya Uviko 19

23 October 2022, 9:40 am

JUMLA ya wananchi 112,669 wamepata chanjo ya UVIKO 19 katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambapo ni sawa asilimia 91ya walengwa ambao ni 123,418 kwa lengo kulinda afya za wananchi wasipatwe na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Akizungumza wakati wa kuhamasisha wananchi wajitokeze kupata chanjo ya UVIKO 19 katika kata ya Mwangata Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa wamefikia asilimia 91ya wakazi wa Manispaa ya Iringa ambapo jumla wanaume 52,053 sawa na asilimia 46.2 na wanawake 60,616 sawa na asilimia 53.8 ndio walimepata chanjo ya UVIKO 19.


Moyo alisema kuwa wamefanikiwa kufikia asilimia hiyo kutokana na ushirikiano walioupata kutoka wadau mbalimbali wakiwamo Wananchi,mashirika mbalimbali ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali (FHI 360),madhehebu ya dini,watu maarufu, viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji ili kuhakikisha wanafanikisha zoezi la wananchi kupata chanjo ya UVIKO 19.

Alisema kuwa wizara ya afya inautaratibu wa kufuatilia magonjwa ya mlipuko yakiwemo yale yanayozuilika kwa chanjo kama vile Surua,Rubella,polio na Pepopunda kwa kuchukua sampuli za wahisiwa wa ugonjwa kwa ajili ya uchunguzi ili kudhibiti magonjwa hayo.

“Ugonjwa huu huathiri watu wa rika zote na hauna tiba,njia kuu ya kuzuia ni kupata chanjo ya UVIKO 19 watu wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kwa lengo la kupata kinga kamili mwilini mwako” alisema Moyo

Moyo alisisitiza wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwa kupata chanjo ya UVIKO 19 kunasaidia kutopata maambukizi ya ugonjwa huo na wale ambao hawajapata  chanjo ya UVIKO 19 wapo hatarini kupata ugonjwa wa Corona kwasababu hawajapata chanjo hiyo.