Nuru FM

Dc Moyo Atoa Siku Saba Kwa Mawakala Wa Mbolea Kufikisha Mbolea Kwa Wakulima

23 October 2022, 9:37 am

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ametoa siku saba kwa mawakala wa pembejeo za kilimo kufikisha mbole aina zote kwa wakulima huku wakisubili serikali kutatua changamoto za kimfumo ambazo wanakabiliana nazo.

 

Akizungumza wakati kikao kazi na wadau,mawakala na kampuni zinazosambaza mbole katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,mkuu wa wilaya Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa wakulima wamekuwa wanalalamika kuwa mbolea haziwafikii mahali walipo kutokana na mawakala kutopeleka mbolea hizo maeneo husika.

 

Moyo alisema kuwa serikali ilishatangaza kuwa wananchi wote waliojiandikisha wanatakiwa kununua mbolea kwa bei ya chini kutokana na serikali kuweka fedha ya ruzuku kwenye kila mfuko wa mbolea ambao mkulima
anataka kununua.

 

Alisema kuwa anatambua kunachangamoto ya kimfumo kutokana na teknolojia ambayo wanaitumia wizara hivyo atawasilisha malalamiko hayo sehemu husika ili watatue changamoto hiyo na wakulima waweze kupata mbolea kwa muda ambao unatakiwa.

 

Moyo alisisitiza kuwa kampuni, mawakala na wadau wa pembejeo za kilimo lazima wazipeleke pembejeo hizo kwa wakulima kwa kuwa wamekuwa wanafanyabiashara ambayo inawalipa na wanapata faida.

 

Alimazia kwa makampuni ya STACCO Tanzania,YARA Tanzania, PREMIUM Tanzania,OCP Tanzania na E.T.G Tanzania yanatakiwa kuongeza idadi ya mawakala wa kusambaza mbolea kwa wakulima ili waweze kuanza maandalizi ya Kilimo.

 

 

Awali akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo, afisa kilimo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Victor Kilatu alisema kuwa baadhi ya mawakala walioteuliwa kuuza pembejeo za ruzuku kutouza pembejeo kwa sababu hawajapewa uwezo wa kuingia kwenye mfumo jambo ambalo linawafanya wachelewe kufikisha mbolea kwa wakulima.

 

Kilatu alisema kuwa kunachangamoto kubwa ya makampuni kushindwa kuwateua mawakala wa kuuza pembejeo na kusababisha kuwa na idadi ndogo ya mawakala ambao wanauza pembejeo za ruzuku jambo ambalo linapelekea
kucheleweshwa kwa pembejeo hizo kufika kwa wakulima.

 

Kwa  viongozi wa makampuni ya kusambaza pembejeo za mbolea STACCO Tanzania,YARA Tanzania, PREMIUM Tanzania,OCP Tanzania na E.T.G Tanzania  waliiomba serikali  kulipa fedha mapema  waendelee kusambaza pembejeo hizo.