Nuru FM

KINANA Ataja Mambo Manne Yaliyokuwa Yakisimamiwa Na Mwalimu NYERERE Ili Kuleta Maendeleo

13 October 2022, 5:27 am

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ametaja mambo manne ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akiyasimamia enzi ya uhai wake kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Kinana ameyataja mambo hayo wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati wa mdahalo kuelekea kumbukizi ya miaka 23 ya hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Akifungua Mdahalo huo Uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Uliokutanisha vyama rafiki vya ukombozi Kusini mwa Afrika, Viongozi mbalimbali pamoja na Wanazuoni, Kinana amesema falsafa ya Mwalimu Nyerere ilijengwa na misingi imara kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania na Bara la Afrika kwa Ujumla.

” Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na maono ya kujua Uelekeo wa Taifa na Wapi Watanzania wanatakiwa kuelekea na hiyo ilitokana na Msimamo wake na kutotetereka,” amesema Kinana.

Kuhusu suala la Uadilifu, Kinana amesema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na misingi ya uadilifu na kwa kujali aliokuwa akiwaongoza ambapo alipenda Uongozi Shirikishi.

“Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na Ushawishi mzuri kwenye Chama na Serikali na hiyo ilisababishwa na uwezo wake mkubwa wa Kujenga hoja kwa ajili ya maslahi ya aliokuwa akiwaongoza,” amesisitiza Kinana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Paul Kimiti ameomba watanzania kuyaendeleza yale yote mema yaliyofanywa na mwalimu ili kulijenga taifa katika misingi imara ya upendo mshikamano na umoja zaidi.

Wakati huo huo Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Profesa Maselino Chijoliga amewakaribisha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kwenda kusoma kozi fupi za uongozi zilizopo katika chuo hicho ili ziwajengee uwezo wa kuongoza vyema kwa maadili ya uzalendo.

Katika hatua nyingine Taasisi ya Mwalimu Nyerere imemkabidhi Komredi Kinana Katiba na Hati ya Usajili wa Taasisi hiyo pamoja Vipeperushi vinayoelezea Historia ya Mwalimu Nyerere kwa Ujumla.

Oktoba 14 mwaka huu itakuwa ni kumbukizi ya miaka 23 ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tangu alipoaga Dunia.