Nuru FM

Wanawake wawili Manyara wakamatwa na misokoto 1220 ya bangi

26 September 2022, 1:47 pm

Kiasi cha misokoto 1220 cha madawa ya kulevya aina ya bangi kimekamatwa hapo jana na jeshi la polisi katika kijiji cha mswakini kilichopo wilayani Babati mkoani Manyara.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoani humo, kamishna msaidizi wa jeshi la Polisi, George Katabazi amesema kuwa misokoto hiyo imekamatwa majira ya jioni na wahalifu wa tukio hilo wametiwa nguvuni.

Watuhumiwa hao ni Beatrice Abel aliyekamatwa akiwa na misokoto 630 na Glory Samwel misokoto 597 wote wakazi wa Ngaramtoni mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo  kamishna, watuhumiwa walipanda basi la kampuni ya KSK lenye namba za usajili T 936 linalofanya safari zake kutoka mkoani Tanga kuelekea mkoani Arusha na walipofika katika kijiji cha mswakini ukaguzi mkali ulifanyika na kuwabaini .

Katika hatua nyingine jeshio la polisi mkoani Manyara linawashikilia watuhumiwa wengine wanne baada ya kukutwa na mali zinazosadikiwa kuwa za wizi, ikiwemo Komputa mbili, tano na laptop mbili na kwamba tayari upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao wa wahalifu wao.

Katika kuendelea kupambana na vitendo vya uhalifu mkoani Manyara, Kamanda Katabazi amesema, kwa sasa msako mkali unaendelea ili kubaini wahalifu wengine ambao wanahatarisha usalama na amani kwa raia pamoja na mali zao na kwamba  wamejipanga vyema.

Pia amewaasa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwa mstari wa mbele kwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kama dalili yeyote ya vitendo hatarishi katika jamii itajitokeza na kulisaidioa jeshi la polisi lifanye kazi kwa urahisi.