Nuru FM

Maafisa Forodha Na Wasimamizi Wa Sheria Mipakani Wapewa Kibarua

17 September 2022, 7:24 am

SERIKALI imewataka maafisa forodha na wasimamizi wa sheria mipakani kuendelea na usimamizi na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt.Switbert Mkama wakati akifungua Mafunzo ya Maofisa Forodha na wasimamizi wa Sheria nchini kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal katika ukumbi wa mpaka wa Namanga, Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya Dkt.Mkama, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt.Catherine Bamwenzaki ametoa rai kwa washiriki hao kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya ozoni kwa wengine ili kuongeza juhudi za kuhifadhi tabaka la ozoni, na hivyo kuokoa maisha duniani.


Serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali zikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuhakiki na kudhibiti uingizaji wa kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni kutoka nje ya nchi pamoja na kuanzisha ubadilishanaji habari kuhusu teknolojia mbadala.

Bamwenzaki alisema kuwa Serikali imehamasisha Watanzania na jumuiya ya wafanyabiashara kuhusu Itifaki ya Montreal na utekelezaji wake na kuanzisha Kitengo cha Kitaifa cha kuratibu juhudi za taifa za kuondosha matumizi ya kemikali zenye kuchangia uharibifu wa tabaka la ozoni.

Tarehe 16 Septemba kila mwaka, Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Miaka 35 ya Itifaki ya Montreal: Ushirikiano wa Kimataifa katika kulinda afya ya binadamu na mazingira” na katika kuadhimisha siku hii shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na kuelimisha kupitia vipindi vya redio na luninga na mitandao ya kijamii kuhusu umuhimu wa kulinda tabaka la ozoni na kuhamasisha umma kuendelea kutumia gesi ambazo ni rafiki kwa tabaka la ozoni.

Pia elimu imetolewa kwa kwa wanafunzi wa fani ya viyoyozi katika Chuo cha Ufundi Arusha pamoja na mafundi wa viyoyozi na majokofu kwa huo kuhusu njia bora za kutumia gesi zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.