Nuru FM

Bodi ya Utalii Kusini Yawahimiza Wadau Wa Utalii Kushiriki Onesho La S!TE

7 September 2022, 6:23 am

Wadau wa Utalii hapa Nchini wametakiwa kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya Utalii yanayojulikana kwa jina la Swahili international Tourism Expo (S!TE) huko Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mkoani Iringa, Afisa kutoka Bodi ya Utalii Kanda ya Nyanda za Juu kusini Bw. Hozza Mbura amesema kuwa Bodi ya Utalii kupitia Wizara ya Maliasili na utalii imeratibu Maonesho hayo ya S!TE ili kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka mataifa mbalimbali katika ukumbi wa Mlimani City.


“Lengo letu ni kuwakutanisha wadau wa utalii kuanzia tarehe 21-23 mwezi wa 10 mwaka huu katika kuadhimisha wiki ya Utalii ili kuwakutanisha wafanyabiashara wa Bidhaa za utalii kutoka mataifa zaidi ya Mia tatu ambapo zaidi ya washiriki mia mbili watashiriki maonesho hayo” alisema Hozza

Aidha Hozza amebainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii wameweka utaratibu kwa wadau wa utalii ambao watashiriki katika maonesho hayo kwa kufanya usajili katika fomu zinazotolewa na Bodi ya Utalii, au katika tovuti ya S!TE.


“Kwa kweli zoezi hili litakuwa likifanyika mara kwa mara ili kuwapata wafanyabiashara wa utalii ambao watashiriki katika maonesho hayo kwa sababu tutawakutanisha na wanunuzi wa bidhaa za utalii na utamaduni ambao wataweza kufanya nao biashara na kukuza uchumi wa nchi” aliongeza Mbura

Hozza amesema kuwa gharama za kushiriki katika maonesho hayo ni kuanzia Dola Mia tatu kutokana na uhitaji wa wadau wa utalii katika vipengele tofauti ambavyo viko siku hiyo.

Amesema kuwa Wadau wa utalii wanaweza kufanya Booking (kuweka nafasi) katika ofisi za bodi ya utalii huku akiwatoa hofu wafanyabiashara hao kujitokeza kwa wingi ili kutangaza biashara zao za kitalii.

Akizungumzia mafanikio ya Maonesho ya Swahili international Tourism Expo (S!TE) Hozza ameainisha kuwa ni kuongezeka kwa wanunuzi kutoka mataifa mbalimbali 14 mpaka kufikia zaidi ya wanunuzi laki tatu ambao wanafika kufanya manunuzi.

Katika hatua nyingine Afisa huyo kutoka Bodi ya Utalii amesema kuwa Bodi ya Utalii kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wameandaa banda kwa ajili ya kufanya maonesho ya vivutio kutoka nyanda za juu kusini katika tukio hilo huko Jijini Dar es salaam.