Nuru FM

Mtendaji na Katibu ‘bandia’ mbaroni kwa uchochezi Mkoani Morogoro

5 September 2022, 5:04 am

Jeshi la Polisi Wilayani Kilosa, limewakamata Mtendaji wa kijiji cha Mambegwa na mtu mmoja aliyejitambulisha kwa cheo bandia cha Katibu wa mwenyekiti wa Kijiji hicho, wakidaiwa kuhusika na uchochezi wa migogoro ya wakulima na wafugaji iliyopelekea watu watano kujeruhiwa baada ya kukatwa mapanga na wafugaji.

Kukamatwa kwa watu hao kunafuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga la kulitaka Jeshi hilo kuwatia nguvuni watuhumiwa hao, wanaodaiwa kushiriki matukio kadhaa ya kuchochea uhasama baina ya pande hizo mbili.

Inadaiwa kuwa, Agosti 31, 2022, wakulima watano walipata madhila yaliyopelekea majeraha miilini mwao, baada ya wafugaji kuvamia katika mashamba yao kwa ajili ya kulishia mifugo yao bila kuhofia na wakati wakihoji kitendo hicho wakashambuliwa.

Baadhi ya wakulima wanaodaiwa kushambuliwa na wafugaji, wakionesha majeraha mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga na Wananchi.

Baadhi ya wananchi wanaeleza usugu wa tatizo hilo kutokea mara kwa mara inachagizwa na baadhi ya viongozi wa kijiji kuhusika.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga amekemea matukio ya namna hiyo, na kuwataka Polisi kuendeleza na msako ili kuwabaini wale wote ambao wamekuwa ni chanzo cha uharibifu na kuvuruga amani.