Nuru FM

IGP Wambura aonya tabia ya kujichukulia sheria mkononi

5 September 2022, 5:06 am

Mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP), Camillius Wambura amewaonya wanachi wa wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro, kuwacha tabia ya kujilichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu wahalifu ikiwemo ama kuwaua, na badala yake wawapeleke kwenya vyombo vya sheria.

IGP Wambura, ametoa onyo hilo wakati akifungua kituo cha Polisi Wilayani humo na kusema kumekuwa na taarifa nyingi za mauaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi, ulevi na wivu wa mapenzi hivyo jeshi la Polisi halitamvumilia uhalifu huo.

”Matukio ya mauaji sababu zake nyingi utaambiwa mgogoro wa ardhi, wivu wa mapenzi na vitu vingine kama hivyo tungeomba muepuke sana hakuna mtu anaruhusiwa kutoa uhai wa mwenzake, huu ni uhalifu ambao uanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema IGP Wambura.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Saimoni Maigwa amesema kituo hicho kitakuwa ni mkombozi kubambana na uhalifu hasa maeneo ya mipakani, na kwamba kimejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na baadhi ya wadau kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi

”Kituo hiki kimejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ambapo jumla ya gharama za ujenzi wa kituo ni millioni 128,796,500 na hadi sasa wananchi wamechangia milioni 34,123,500 kwa kufanikisha ujenzi kuanzia msingi hadi boma kukamili kwa kutoa fedha taslimu na wengine wakichagia vifaa vya ujenzi.”