Nuru FM

WAZIRI MAJALIWA AWAPONGEZA WADAU WALIOCHANGIA SH. BILIONI 1.26 KWA TIMU ZA TANZANIA

25 August 2022, 7:31 am

WADAU wa michezo nchini wamechanga jumla ya sh. bilioni 1.26 ili kuzisaidia timu za Serengeti Girls na Tembo Warriors ambazo zinatarajia kushiriki michuano ya kimataifa huko India na Uturuki.

 

Akizungumza mara baada ya kupokea ahadi na michango ya wadau hao, kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema michango waliyoitoa inaleta ujumbe kuwa wanataka makombe ya dunia yaje Tanzania.

 

Mbali ya michango ya fedha, wadau hao wameahidi kulipia tiketi za safari kwa timu zote mbili, kulipia bima kwa wachezaji wa timu zote mbili, kutengeneza na kuzibrand jezi na tracksuit, kununua viatu na soksi kwa wa timu zote mbili.

Waziri Majaliwa amewashukuru wadau wote kwa michango yao na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuthamini michango waliyoitoa.

 

Michango hiyo imetolewa na wadau kutoka sekta za fedha/mabenki, mitandao ya simu, viwanda, taasisi za Serikali, vyombo vya habari, wadau binafsi na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

 

Naye Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa amesema ili timu hizo zipate maandalizi ya kutosha zinahitajika shilingi bilioni 3.76 ili kugharimia timu zote mbili ambapo kati ya hizo, Serengeti Girls inahitaji sh. bilioni 2.57 na Tembo Warriors inahitaji sh. bilioni 1.19.

Amesema timu ya soka ya watu wenye ulemavu ya Tembo Warriors ambayo tayari iko kambini inatarajiwa kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia Oktoba, mwaka huu na ile ya Serengeti Girls inatarajiwa kushiriki mashindano yake nchini India, Novemba mwaka huu.