Nuru FM

KAMPUNI YA MAXCOAL KUZALISHA MAFUTA NA GAS MKOANI NJOMBE

25 August 2022, 7:33 am

Kampuni ya uchumbiji madini ya makaa ya mawe maximum Energy and Minerals Limited (MAXCOAL)  iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe imeadhimia kuanzisha uzalishaji gas na mafuta kwa kutumia makaa ya mawe pindi watakapokamilisha taratibu za kiserikali.

 

Akizungumza hayo mwenyekiti wa makampuni ya Maxcoal hapa nchini Liginiko Chale amesema malengo yao ni kuzalisha mafuta ya disel mapipa 12,000 kwa siku, petrol mapipa 8,000 pamoja na gas itakayotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya  matumizi ya kiwanda chao pamoja na mradi kwa ujumla.

Chale amesema katika kuzalisha umeme wanatarajia kuzalisha MW 250 huku mahitaji yao ni MW 200 hivyo MW 50 zitakazobaki wanategemea kuziingiza katika mfumo wa serikali japo endapo serikali itaridhia wangehitaji wananchi wa vijiji vinavyozunguka mradi wapatiwe umeme huo pasipo malipo yoyote.

 

“Ni matamanio yetu kuona vijiji vilivyo jirani na mradi wetu vinanufaika na umeme utakaozalishwa hapa kwa kupatiwa bure kabisa, japo kupatiwa huko umeme kunategemeana na maamuzi ya serikali”.

 

Sanjari na hilo mwenyekiti huyo amesema kampuni hiyo inamiliki eneo la Sqkm. 54 ambazo tayari zimeshafanyiwa utafiti na kuthibitishwa na wataalamu waliothibitishwa na bodi ya Majiolojia ya Australia na Canada ambapo kwa tafiti zao waligundua eneo hilo lina makaa ya mawe tani Ml. 519.

 

Ameongeza kuwa kwa sasa bado mitambo inaendelea na kufanya tafiti ili kuweza kugundua endapo kuna hazina ya madini zaidi ya makaa ya mawe.

 

Hata hivyo amesema mradi huo ulianzishwa mwezi Julai 2021 ambapo tokea kipindi hicho walikuwa wanatengeneza miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja hivyo kwa sasa wanatarajia kuanza kusafirisha makaa hayo katika makampuni mbalimbli.

 

Aidha kwa upande wake Meneja mradi wa kampuni hiyo Eng. Vicent Malima amesema mpaka sasa watanzania zaidi ya 60 wameweza kupatiwa ajira na tayari wameandaa macamp ambayo ujenzi wake unaendelea.

 

Amesema camp hizo zitakuwa na nyumba 10 zenye jumla ya vyumba 50 hivyo zitakapokamilika zitasaidia kumudu idadi ya wafanyakazi watakao endelea kuongezeka mgodini hapo.

 

Mradi huo upo katika kata ya Ibumi kijiji cha Masimavalafu kinachopakana na kijiji cha Liugahi kilichopo katika kata ya Luilo, na unamilikiwa na wawekezaji wa kitanzania.