Nuru FM

Jeshi la polisi Lindi lawadaka watu kumi kwa tuhuma za wizi na usafirishaji mihadarati

13 August 2022, 7:44 am

Jeshi la polisi mkoani Lindi linawashikilia watu kumi kwa tuhuma za wizi na usafirishaji mihadarati.

Hayo yameelezwa na kamanda wa polisi wa mkoa (RPC) wa Lindi, Kamishna msaidizi wa polisi (ACP) Marco Chirya alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya mkoa ya jeshi hio iliyopo katika manispaa ya Lindi.

Kamanda Chirya alisema kufuatia matukio ya wizi wa pikipiki ya mara kwa mara ambayo yalionesha dalili za kuongezeka, jeshi la polisi mkoani Lindi lilianza kufanya msako katika wilaya zote zinazounda mkoa wa Lindi. Msako ambao ulianza tarehe 1.08.2022 na kumalizika tarehe 9.08.2022.


Alisema zoezi hilo( oparesheni) lilifanikisha kuwatia mbaroni watu kumi ambao wanatuhumiwa kutenda vitendo vya uhalifu. Ikiwemo kuvunja na kuiba pikipiki, kunyang’anya pikipiki, kuvunja na kuiba vifaa mbalimbali na usafirishaji wa mihadarati.

Kamanda Chirya alivitaja vitu vilivyokamatwa kupitia msako huo kuwa ni pikipiki tisa,Televishen aina ya sharp ya nchi 43 moja, simu za aina tofauti 13 na mihadarati aina ya bangi kilo 44 na gramu 100.

Alisema bangi na televisheni vimekamatwa katika wilaya ya Nachingwea, pamoja na pikipiki tatu. Huku pikipiki nne zilikamatwa katika wilaya ya Ruangwa, na pikipiki mbili zilikamatwa wilayani Lindi.

Ofisa huyo wa juu wa jeshi la polisi mkoani Lindi kilo hizo 44 na gramu 100 zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kutoka Nachingwea kwenda Dar-es-Salaam.

Kuhusu bangi kamanda Chirya amewataka madereva na wasaidizi wao wahakikishe kwa kuanza kukagua ili wathibitishe ina bidhaa gani badala ya kupokea na kusafirisha bila kukagua.

Aidha kamanda Chorya alibainisha kwamba wizi wa pikipiki una njia tofauti zinazo tumika kufanikisha. Kwani kuna watu wanavunja na kuchukua, kuna watu wanaoiba zikiwa kwenye maegesho na wengine huwakodi madereva pikipiki( madereva wa bodaboda) wanapowafika maeneo ya mbali na makazi ya watu humuamrisha dereva asimamishe pikipiki, ndipo wahalifu wengine hujitokeza na kumnyang’anya baada ya kumpiga na hata kumuuwa dereva boda boda.

” Nitoe wito kwa madereva boda boda wasikubali kuwasafirisha watu wasio wajua. Lakini pia washirikiane na wachukue namba za simu za wanaowasafirisha na kuwapa wenzao ili wajue anamsafirisha nani na anakwenda wapi,” alisema kamanda Chirya.

Kamanda huyo alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha wanaolima bangi, wezi na wanyang’anyi kwamba zoezi hilo ni endelevu na jeshi hilo lipo macho muda wote.

Alikwenda mbali kwakusema wahalifu wasijisumbue kuhama mkoa. Kwani watafutwa kokote watakako hamia. Huku akiwaonya wanaomiliki mashamba ya bangi wajandae kukamatwa kwani taarifa zao kamili zipo mezani kwake.

Aliwataka wamiliki hao wa mashamba ya bangi wasipoteze muda na kusubiri kukamatwa bali wajisalikishe wenyewe badala ya kusubiri maumivu makali watakayo pata iwapo jeshi hilo litawafuata walipo.

Kuhusu kinachoendelea dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa, alisema wanaandaliwa mashtaka ili wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka hayo.

Mbali na hayo kamanda Chiry alitoa wito kwa wananchi waliibiwa vifaa vilivyokamatwa( Pikipiki, televisheni na simu waende wakazitambue katika ofisi ya mkoa ya jeshi hilo.