Nuru FM

Waziri Mabula Awaonya Viongozi Wa Vijiji Na Vitongoji Ambao Ndio Vinara Wa Kuchochea Migogoro Ya Ardhi

11 August 2022, 7:41 am

WAZIRI wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula ametoa onyo kwa baadhi ya Viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji wanaokuwa chachu ya migogoro kwa kuuza ardhi zaidi ya mara moja ili kujinufaisha matumbo Yao Hali inayosababisha ongezeko la migogoro ya ardhi.

Vilevile ameeleza, Mkoa wa Pwani ni Mkoa wenye fursa nyingi za kimaendeleo na kiuchumi lakini changamoto kubwa ni  migogoro ya ardhi, ambayo inapaswa kuvaliwa njuga ili kupata ufumbuzi.


Waziri Angelina alitoa onyo hilo Mara baada ya kuwakabidhi ripoti  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge  na  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah ripoti iliyoandaliwa  kuhusu migogoro ya ardhi ya kata ya Mapinga ili iweze kufanyiwa kazi.

Aliwaasa viongozi wote wa vijiji na vitongoji kuacha mara moja kujivika mamlaka kinyume na taratibu za sheria na wanatengeneza miliki bandia ili kujipa kipato.

Aliendelea kusema ” uvamizi wa ardhi ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo hawatakuwa tayari kuona shamba la mtu linavamiwa  kisa ni shambapori.”

Pia Mabulla alishauri wananchi kutokufanya maamuzi ya haraka  bila kufika Halmashauri husika  na kufuata taratibu.

Nae mwanakamati  Peter Richard Matagi  kiongozi mkuu wa tume iliyoundwa kwaajili ya kuandaa ripoti na kushughlikia migogoro hiyo alipata fursa ya kuwasilisha  mrejesho mfupi kuhusu agizo walilopewa na Waziri kuhusu migogoro ya ardhi ikiwemo baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kutumia mamlaka zao Kuwa chachu ya vyanzo vya migogoro ya ardhi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Abubakari Kunenge alipokea  ripoti hizo na kuwasisitiza wananchi  wa Mapinga  kuwa makini na wasikubali   kupewa suluhisho kwa mdomo bali masuluhisho yawe  kwa maandishi.

Kunenge aliwatoa hofu wananchi wa kata ya Mapinga na kuhakikisha analibeba tatizo linalowakabili, “niwahakikishie Ili si la mkuu wa Wilaya bali la kwangu ” alisema Kunenge.

“Kuhusu suala la haki “watu wengine  kwa makusudi  wanakuja  kuleta  kero bila sababu kwa kutokuzingatia sheria hakuna aliyejuu ya  sheria  .”Mhe. Waziri nikuhakikishie watu  wawe na utulivu  nitapitia na tutaona mapendekezo tofauti na tutaangalia njia bora  zaidi ya kutatua , haki ya watu haitapotea ” alisema Kunenge.

Kunenge alisisitiza  wale wote wanaovunja  sheria watashughulikiwa ” hamtobaki salama sisi hatuna maneno mengi.”alisema Kunenge.