Nuru FM

Dc Kiswaga Atumia Mchezo Wa Bao Kuhamasisha Wananchi Kujitokeza Siku Ya Sensa

12 July 2022, 4:49 pm

WANANCHI wa wilaya ya Iringa wametakiwa kujitokeza kuhesabiwa siku ya SENSA ili kutengeneza taswira halisi ya serikali kujua idadi ya wananchi kwa lengo la kuwapelekea maendeleo kulingana na idadi iliyopo kila eneo.

Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga na kuongeza kuwa wananchi watakiwa kujitokeza siku SENSA ili waweze kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo yao.

Kiswaga aliwata viongozi mbalimbali kutumia fursa ya uwepo wa michezo kwenye vijiji, mitaa, kata na tarafa kuhamasisha wananchi wajitokeze kuhesabiwa.

Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga akiongea na wananchi kuhusu umuhimu wa SENSA ya watu na makazi kwa wananchi wa Tarafa ya Pawaga

Alisema kuwa kwenye kila mchezo kunakuwa na kundi kubwa la wananchi hivyo ni rahisi sana kufikisha ujumbe wa SENSA na ujumbe ukapokelewa vizuri.

Kiswaga alisema kuwa mchezo wa Bao la solo limekuwa kiunganishi kikubwa kwa wananchi na serikali kama ambavyo hayati Mwl. Nyerere alitumia mchezo huo katika harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika na kufaulu kuupata uhuru huo.

Hivyo michezo yote inatakiwa kupewa kipaumbele sawa ili kuiweka jamii ya wanamichezo pamoja na kutumia fursa za michezo kwa maendeleo ya taifa.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kucheza mchezo wa bao mbele ya mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga juu ya umuhimu wa SENSA ya watu na makazi

Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa vijana wilaya ya Iringa vijijini, Makala Mapesa alisema kuwa mchezo wa bao la solo ni mchezo ambao unachezwa na watu wa lika zote kwa ajili ya fursa na kutengeneza fursa za kimaendeleo wakiwa wanacheza mchezo huo.

Mapessa alisema kuwa mchezo wa bao la solo umekuwa moja ya michezo ambayo unatakiwa kutumia akiri nyingi na maarifa kuliko kutumia nguvu hivyo ukicheza mara kwa mara mchezo huo akili yako itachangamka kwenye kufikiri.

 

CREDIT FRED MGUNDA