Nuru FM

Wanafunzi wafa kwa kukosa hewa ndani ya ‘School Bus’

11 July 2022, 8:24 am

Dereva wa basi la shule, Odunsa Mandala anashikiliwa na Polisi baada ya wanafunzi wawili kufariki huku wengine wakizimia kutokana na kukosa hewa katika basi lao la shule eneo la Aguda katika jimbo la Lagos.

Mandala, alikuwa akiendesha basi kuwarudisha wanafunzi makwao baada ya kufungwa kwa shule wakati kisa hicho kilipotokea Julai 8, 2022, na ndipo Wanafunzi walimlalamikia mara kadhaa kuhusu jinsi walivyokosa hewa lakini alidaiwa kupuuza hadi wengi wao walipozimia.

Inadaiwa kuwa, mara baada ya kuona hali hiyo, alichukua hatua ya kupiga simu kuomba msaada na ndipo wanafunzi hao wakakimbizwa hospitali ya Randle iliyopo jimboni Lagos ambapo wanafunzi wawili walipoteza maisha.

Msemaji wa polisi wa jimbo la Lagos, SP Benjamin Hundeyin, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo amesema, “Ndio, dereva amekamatwa lakini roho za vijana tayari zimeondoka, ni huzuni.”

Amesema, “Dereva wa basi la shule alipuuza malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa watoto aliokuwa akiwapeleka nyumbani kwamba hawakuwa wakijisikia vizuri, na baadhi ya watoto walipoteza fahamu na wawili walikufa.”

Hata hivyo, Msemaji huyo amezitaka Shule zijitahidi kuongeza wigo katika kuajiri na kuzingatia kanuni za kazi ikiwemo kuongeza idadi ya vyombo vya usafiri, huku akiwataka Wazazi kufanya ukaguzi wa kina katika wa shule za awali zile za msingi kabla ya kuwakabidhi watoto wao kwa walimu.

Hospitali ya Randle iliyopo jimboni Lagos ambapo wanafunzi wawili walipoteza maisha mara baada ya kufikishwa hapo kwa matibabu ya kukosa hewa.