Nuru FM

COSTECH Yafadhili Mradi Wa Unenepeshaji Ng’ombe Nchini.

24 June 2022, 8:00 am

TUME ya Taifa Sayansi na Teknolojia ( COSTECH), imetoa zaidi ya sh milioni 400 kwa ajili ya Miradi miwili mojawapo ukiwa wa Uandaaji wa Lishe Bora ya Gharama Nafuu kwa Unenepeshaji Ng’ombe nchini.

Aidha Mradi mwingine ni ukarabati wa maabara ya utengenezaji na tathmini ya chakula cha Ng’ombe katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania ( TALIRI), Kanda ya Mashariki Kituo cha Tanga.

Akizindua Mradi huo wa Uandaaji wa Lishe Bora ya Gharama Nafuu kwa Unenepeshaji Ng’ombe nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Mifugo Tixon Nzunda aliipongeza COSTECH kwa ufadhili huo walioutoa kwa TALIRI Tanga.

Nzunda alisema Mradi huo uliofadhiliwa na COSTECH lengo lake ni kupata lishe sahihi kwa ajili ya kuongeza ubora wa nyama Tanzania.

Pia ukuzaji na uendelezaji kibiashara Teknolojia ya lishe ya Unenepeshaji Ng’ombe nchini ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa wadau wa tasnia ya nyama nchini.

Awali Meneja Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia, Ntufye Mwakigonja alisema kuwa Mradi wa maabara uliogharimu sh milioni 307, na Mradi huo wa uandaaji wa lishe bora sh milioni 120.

” Fedha hiyo iliyotolewa kwa Mradi huo wa uandaaji wa lishe bora ya Gharama nafuu kwa Unenepeshaji ng’ombe pia imenunua ng’ombe 30 pamoja na kujenga eneo la majaribio ya Ng’ombe wananenepeshwa kupitia chakula hicho,” alisema.

Aliongeza kuwa fedha hizo pia zimetumika kulima ekari 12 za mahindi ambayo yametumika kutengenezea lishe.

” COSTECH inaigusa sekta ya Mifugo kuzingatia eneo la mapishi kwani mwaka 2020 ilipeleka SUA sh milioni 70 kwa ajili ya kubaini changamoto ya malisho ya Ng’ombe eneo la Ranchi ya Kongwa Dodoma, ambapo malisho yalivamiwa na gugu kongwa,” alisema.

Aliongeza kuwa pia COSTECH ilitoa sh milioni 400 kwa Kituo cha TALIRI Mpwapwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Profesa Erick Komba alieleza majukumu ya Taasisi hiyo kuwa ni kusimamia, kuratibu na kufanya tafiti za Mifugo upande wa Tanzania Bara.

Vile vile kubaini, kutathmini na kusambaza Teknolojia bora za Mifugo.

Alitaja maeneo ambayo TALIRI inafanya utafiti kuwa ni vyakula vya Mifugo, malisho, mbari za Mifugo, uzalishaji, uzazi, afya ya Mifugo, Tabia za Mifugo na haki za Mifugo.