Nuru FM

Sabaya: Mungu amenitendea miujiza

11 June 2022, 8:09 am

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amemshukuru Mungu kwa kumfanyia miujiza iliyopelekea kushinda kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili.

“Mimi ninamshukuru Mungu sana na ambariki Rais aliyeweka mfumo wa haki inawezekanaameshafanya kwa wengi lakini Mungu kupitia kwa watu mbalimbali tayari amenitendea miujiza,” alisema Sabaya.

Mbali na Sabaaya washtakiwa wengine walikuwa ni John Aweyo, Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, Sylvester Nyegu, Nathan Msuya na Jackson Macha, ambao kwa pamoja wameshinda kesi baada ya ushahidi uliotolewa na Jamhuri kuwa na mapungufu.

Hata hivyo, Sabaya ataendelea kubaki mahabusu kwa kuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, sambamba na wenzake Sylvester Nyegu, Nathan Msuya na John Aweyo.

Juni 10, 2022 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, alitoa hukumu ya kumuachia huru Sabaya na wenzake, ikiwa ni kesi ya pili kushinda.

Mei 6, 2022 Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, ya kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yao ya kwenda miaka 30 jela.