Nuru FM

Wafanyakazi wa Nuru Fm Watoa msaada kwa wafungwa Iringa

21 May 2022, 11:28 am

Wafanyakazi wa Redio Nuru fm wakishirikiana na watuma salamu Mkoa wa Iringa wamewatembelea wafungwa wa Gereza la iringa manispaa na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali.

Wakizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo yakiwemo mablanketi, mashuka, nguo, mafuta ya kupaka, sabuni za kufulia na kuogea, taulo za kike na dawa za meno Meneja wa Nuru fm Victor Chakudika amesema kuwa msaada waliotoa una thamani ya shilingi milioni 3.3 na wameshirikiana na wadau wengine.

Awali Mratibu wa zoezi Hilo isaack kikoti amesema kuwa wameamua kuwathamini wafungwa kwa kuwapelekea mahitaji hayo huku akiwashukuru wadau waliojitokeza kufanikisha jambo hilo.

Kwa upande wake Mstahiki Meya Manispaa ya iringa Ibrahim Ngwada ambaye alishiriki katika zoezi hilo amewapongeza Nuru fm kwa kuwatembelea wafungwa huku akikiri kuwa bado wafungwa wanauhitaji wa kupata huduma hizo.

Amesema kuwa baraza la madiwani halmashauri ya manispaa ya iringa limejifunza kuwa na moyo wa kuwakumbuka watu wenye mahitaji kupitia redio Nuru Fm kwani wamekuwa na muendelezo wa kurejesha kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Gereza la Iringa, insepkta Dickson Joel Mwaihojo amewashukuru wafanyakazi wa Nuru fm wakiwa na watuma salamu na wadau wengine kwa kujitokeza kuwapatia msaada huo ambao utapunguza changamoto za wafungwa.

Naye mwenyekiti wa watuma salamu mkoa wa Iringa Wiliam kitosi amesema kuwa wameungana wafanyakazi wa Nuru fm ili kuwaapatia msaada wafungwa hao kwa kuwa ni kundi ambalo limesahaulika katika jamii.

Nuru FM kupitia kipindi cha kiyoyozi ilikuwa na wazo la kutembelea wafungwa na ndipo wakaanzisha kampeni ya BADO TUPO NA WEWE NA KUTHAMINI yenye lengo la kukusanya fedha na mahitaji mengine kutoka wadau na marafiki wa Kituo hiki ili kuwapatia mahitaji hayo.

Miongoni kwa wadau walioshiriki katika tukio hilo ni pamoja na watuma salamu mkoa wa iringa, Bateleur safari & tour, Nuru Fm, Uongozi wa sun Academy, Asali Murua, dream Life na wasikilizaji wa Nuru FM.