Nuru FM

Polisi Ruvuma Na Tawa Wakamata Meno 9 Na Vipande 8 Vya Meno Ya Tembo

14 May 2022, 8:25 am

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana  na Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori (Tawa) kanda ya kusini, limewakamata watu watatu wakazi wa wilaya ya Tunduru wakiwa na meno tisa na  vipande vinane vya meno ya Tembo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishina msaidizi Joseph Konyo aliwataja watu hao kuwa ni Said Awadi,Hassan Hakimu na Zakaria Rashid  na walikamatwa tarehe 10 Mei 2022 majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha Milonde-Kiuma.

Kamanda Konyo alisema,meno  hayo yana uzito wa kg 20.4 na thamani yake ni Sh. milioni 138,600,000 ambapo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

Aidha Konyo alisema,Jeshi la Polisi na askari wa Tawa wamefanikiwa kukamata  meno Matano ya Tembo yenye uzito wa kg 44 yenye thamani ya Sh.103,950,000.

Alisema,meno hayo yalikamatwa katika kijiji cha Hanga- Monastery wilayani Namtumbo, baada ya kutelekezwa na watu ambao walistukia mtego uliowekwa na Polisi na askari wa Jeshi la Uhifadhi,hata hivyo jitihada za kuwatafuta na kuwakamata  zinaendelea.

Kwa mujibu wa Kamanda Konyo,jumla ya Tembo saba waliuawa katika matukio hayo mawili na kila tembo mmoja ana thamani ya Dola za  Kimarekani  1,500 sawa na pesa za Kitanzania  Sh.milioni 242,550,000 kwa Tembo wote.

Alisema,kupatikana kwa nyara hizo na kukamatwa kwa watu hao kunatokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori(Tawa).

Kwa upande wake Kamishina msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori(Tawa)kanda ya kusini Abraham Jullu,amewataka wananchi kuepuka vitendo vya uwindaji haramu wa wanyamapori wakiwamo Tembo ambao ni rasilimali na tunu kubwa za Taifa.

Alisema,uvunaji(uwindaji) haramu wanyamapori ni kosa kisheria kwani wanyama hao wanalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuvutia  wageni na Watanzania wanaokwenda kutembelea Hifadhi za Taifa na kutoa fedha ambazo zinazochangia kukuza uchumi wa nchi yetu.

Alisema,Tawa na  vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitahakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakojihusisha na vitendo vya uwindaji haramu.

Kamishina Jullu, ameitaka jamii kusaidiana na mamlaka husika kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,badala ya kutanguliza maslahi binafsi.

Katika hatua nyingine Kamanda Konyo alieleza kuwa,kuanzia tarehe 1 hadi 12 Mwezi huu Jeshi hilo limefanya operesheni maalum iliyolenga kuwakamata watu wanaojihusisha na matukio ya uvunjaji,wizi na wapokeaji wa mali za wizi katika  maeneo mbalimbali.

Kamanda Konyo alisema,katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kumi na sita kati yao wanaume kumi na tatu  na wanawake watatu wakiwa na vitu vya wizi.

Alitaja vitu vilivyokamatwa ni Televisheni kumi,Radio Subwofer nne,spika moja,magodoro mawili,mitungi mitano ya Gesi,viti vya Plastiki kumi,ndoo hamsini za mafuta ya kula,kitanda,mabegi ya nguo na baiskeli moja.

Ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na shughuli za ujangili na matukio ya wizi kuacha mara moja, kwani Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama havitawafumbia macho.