Nuru FM

Naibu Waziri Ridhiwani Awataka Watendaji Sekta Ya Ardhi Kutenda Haki

14 May 2022, 8:32 am

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanatoa haki wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.

Alisema, utoaji haki uko katika sura tofauti kuanzia zoezi la utoaji hati, upatikanaji haki katika mabaraza ya ardhi na nyumba sambamba na utoaji taarifa na uwezeshaji wananchi katika ardhi au rasilimali ardhi.

Alisema, baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wamekuwa miungu watu kwenye maeneo yao kuliko hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ardhi yote iko chini ya mamlaka yake na kubainisha kuwa, mwananchi anaweza kwenda ofisi ya ardhi kwa ajili ya kumilikishwa ardhi lakini adha anayoipata wakati wa kuomba kupata uhalali wa kumiliki ardhi yake basi maafisa ardhi wamekuwa wakijizungusha bila kumsaidia.

‘’kama nilivyokwisha sema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, uabaishaji ufike mwisho  tumeelewana ndugu zangu’’ alisema Rdhiwani.

Naibu Waziri Kikwete alieleza hayo tarehe 13 Mei 2022 alipokutana na watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mbeya ambapo alioneshwa  kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya watumishi wasiowaadilifu.

‘’Kama kuna mtumishi anadhani kuna suala la kula kula ovyo kwenye Wizara hii ya ardhi basi siyo kwa nyakati hizi, ndugu zangu watendaji wenzangu naomba tuwe waadilifu katika kutenda haki kwa wananchi.’’ Alionya Ridhiwani Kikwete  Naibu Waziri Wizara  ya Ardhi.

Sambamba na hilo aliwataka Maafisa Mipango miji wa Mkoa wa Mbeya kuwa na mipango bora ya mipango miji ili jiji Mbeya lisiendelea kuwa jiji la makazi holela.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, ukiwa kwenye ndege unaona milima ya mbeya imejengwa majengo kwenye ardhi isiyopimwa ambapo aliwataka Maafisa Mipango Miji hao kutosubiri watu kuendeleza makazi holela na baadae kujitokeza kurasimisha maeneo hayo.

‘’Acheni kusubiri wananchi wajenge alafu nyie muwafuate kuendeleza mipango miji badala yake muwe wa kwanza kupima na kupanga miji ili wanachi waishi kwenye makazi bora tofauti na sasa mnapowaa na kusababisha kuaribu milima na taswira ya jiji la Mbeya’’ alisema Ridhiwani.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete yuko mkoani Mbeya kwa ziara ya siku mbili ambako mbali na na kufanya kikao na watumishi wa sekta ya ardhi ameshiriki zoezi la utoaji hati na leseni za makazi kwa wananchi wa halmashauri ya jiji la Mbeya pamoja na wale wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi.