Nuru FM

Tuzo za Waandishi wa habari Nchini kutolewa Mei 3

20 April 2022, 7:29 am

Wanahabari wa Tanzania wanatarajia kupata tuzo kwa makundi tofauti katika tasnia hiyo ikiwa ni katika kuenzi na kutambua umuhimu wao katika kuleta maendeleo ya nchi kitaifa na kimataifa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Rodney Thadeus Mbuya, wakati wa mkutano na waandishi wa Habari  jijini Dodoma.

Tuzo hizo ambazo zinatarajiwa kutolewa Mei 3, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari duniani yatakayofanyika Jijini Arusha zitatolewa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbuya amesema Tuzo takribani kumi na mbili zitatolewa kwa wanahabari ikiwemo tuzo ya Jamii, tuzo ya sayansi na technolojia, tuzo utalii na uwekezaji, tuzo ya wamiliki bora wa vyombo vya habari, tuzo ya michezo na burudani, tuzo ya mwandishi chipukizi.

Pia tuzo ya mwanahabari mwanamke mwenye mafanikio katika sekta ya habari, tuzo ya Vyombo vya Habari vya kidijiti, tuzo ya ushirikiano kwa wadau wa Habari, tuzo ya Maendeleo Endelevu, tuzo ya mtangazaji bora wa Taasisi za Serikali na Umma.

Ameongeza kuwa kutakuwa na tuzo nyingine kubwa ‘Tanzanite Award’ ambayo inatarajiwa kutolewa kwa Kiongozi mkubwa ambaye amechangia kuleta mabadiliko katika Sekta ya Habari.

Kwa upekee wa Maadhimisho ya mwaka huu, Maadhimisho haya yatakuwa ni ya Kimataifa ambapo wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi watashiriki na Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni ‘Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidijiti’ na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Miongoni mwa Wadau watakaoshiriki ni Chama cha Wahariri kutoka nchi za Afrika Mashariki, Wadau mbalimbali nchini na wawakilishi kutoka nchi za Afrika.