Nuru FM

Wavuvi Watakiwa Kuacha Kufanya Kazi Kwa Mazoea Kuepuka Vifo, Kupoteza Mali

9 April 2022, 7:41 am

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesisitiza umuhimu wa wavuvi kuzingatia usalama ikiwemo kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea wanapokuwa katika shughuli za Uvuvi wawapo majini ili
kuwaepusha na vifo,majeruhi na kupoteza mali.

Huku wakisisitiziwa umuhimu wa kuwa na vifaa vya kujiokolea wanapokuwa majini ili viweze kuwasaidia kuepukana na ajali ambazo wanaweza kukumbana nazo.

Wito huo ulitolewa leo na Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua wakati na akizungumza na wavuvi, wamiliki wa vyombo, manahodha na wananchi wa Vijiji vya Monga Vyeru wilayani Mkinga na Mwalo wa Sahare Jijini Tanga mkoani Tanga walipokwenda kutoa elimu ya umuhimu wa usalama na utunzaji wa mazingira.

Alisema kwamba ni muhimu kwao kuweza kuhakikisha wanazingatia usalama wakati wanapokwenda kufanya shughuli zao kwani hilo litawaepusha na majanga ambayo wanaweza kukutana nayo na kupelekea kupata majeraha au kupoteza maisha na mali.

“Serikali imeona hilo ni jambo la msingi sana na ndio maana tumeona leo tuje hapa Monga Vyeru kuwapa elimu hii ya usalama  na utunzaji wa mazingira hususani mnapokuwa kwenye shughuli zenu hili ni jambo hilo lakini pia kuhakikisha mnakuwa na vifaa vya uokozi”Alisema

“Kwani tunatambua kwamba pia wavuvi wana familia hivyo elimu hii itaweza kuwasaidia kupunguza ajali,kuondoa vifo na kupunguza majeruhi na kuacha familia kuwa tegemezi”Alisema

Afisa Mfawidhi huyo alisema shughuli za usalama sio jambo la mtu mmoja bali ni watu wote hivyo lazima wahakikisha wanazingitia sheria za usalama ikiwemo kuvaa majaketi ya kujiokolea “life jacket” ili yaweze kuwasaidia pindi wanapokumbana na dhoruba baharini waweze kujiokoa.

Hata hivyo alisema ni muhimu na vizuri kwa wenye vyombo vinavyotumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi wanakuwa na watu wenye ujuzi na kufanya kazi za majini ikiwemo wajibu wa mmiliki kutii sheria bila shuruti kuhakikisha usalama wake.