Nuru FM

TBS Yatoa Jumla Ya Leseni Na Vyeti 211 Kwa Wajasiriamali Wadogo

9 April 2022, 7:32 am

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) imeweza kutoa jumla ya vyeti na leseni mia mbili kumi na moja (211) na Kati ya hizo, leseni na vyeti mia moja kumi na tano (115) sawa na (55%) vilitolewa kwa wajasiriamali wadogo.

Aidha Shirika limetoa leseni na vyeti tisini na sita (96) sawa na 45% kwa wazalishaji wengine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utoaji leseni na vyeti, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Bi.Viola Masako amesema Vyeti na leseni hizo vinahusisha bidhaa mbalimbali kama vile chakula, vipodozi, viatu, vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, vifaa vya makenika, magodoro, vibebeo pamoja na vifungashio.

Amesema katika kuunga jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi hasa kupitia sekta ya viwanda, Shirika limeendelea kutenga bajeti ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata leseni ya kutumia alama ya ubora katika bidhaa zao bure.

“Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Shirika limetenga jumla ya Shilingi milioni mia mbili hamsini na sita (256,000,000) za Tanzania kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo”. Amesema

Pamoja na hayo ametoa wito kwa wajasiriamali nchini kuchangamkia fursa iliyotolewa na Serikali kwa kuanzisha viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na viwanda hivyo vitengeneza ajira kwa watanzania na Serikali itapata kodi ambayo itatumika kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi.