Nuru FM

Shilingi bilioni 93.1 zatumika kwenye miradi ya mendeleo Iringa

5 April 2022, 8:20 am

Sh93.1 bilioni zimetumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Iringa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kihesa Kilolo – Igumbilo itakayosaidia kupunguza msongamano wa magari mjini.

Kwa sasa magari yote yanapita katikati ya mji na kusababisha msongamano mkubwa kutokana na ukosefu wa barabara mbadala.

Akizungumzia miaka 100 ya uongozi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kikao chake na viongozi wa dini pamoja na Baraza la Wazee la Manispaa ya Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo amesema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea.

“Ikitokea roli likapata ajali mlima wa Ipogoro na kuziba barabara hali lazima iwe tete, lakini Serikali imetoa Sh7.75 bilioni kwa ajili ujenzi wa barabara hii,” amesema.

Amesema shughuli zinazofanyika kwa sasa ni ujenzi wa madaraja na barabara kwa mita 450.

Moyo amesema fedha nyingine zimetumika kwenye kuboresha miradi ya elimu, afya, ujenzi wa uwanja wa ndege, machinjio ya kisasa, sekta ya umeme na biashara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya amesema kazi zilizofanyika zitasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwenye mji huo.

“Tunaona kwa macho kazi zilizofanyika, niipongeze Serikali lakini nikupongeze DC kwa kuzungumza haya mbele ya wazee. Vijana wanaweza kukimbia lakini wazee wanaijua njia, tuwasikilize,” amesema.