Nuru FM

Wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shule kufikishwa Mahakamani

31 March 2022, 4:58 pm

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda ametoa mwezi mmoja kwa Wazazi na Walezi wa wanafunzi 16 wa Tarafa ya Shelui ambao hadi sasa hawajaripoti shuleni baada ya kufaulu darasa la saba kwenda Sekondari kuhakikisha wanafanya hivyo na atakae kaidi agizo hilo hatua kali zakisheria zitachukuliwa dhidi
yake.

Mwenda ametoa agizo wakati akiwahutubia  Wananchi wa Tarafa ya Shelui kwenye mkutano wa hadhara baada ya  kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo  kumaliza kukagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Tarafa hiyo.

Serikali haiwezi kuvumilia kuona wanafunzi waliofaulu kwenda kuanza Sekondari hawaendi shuleni licha ya kutumia fedha nyingi ya kuboresha mazingira bora ya kupata elimu hivyo naagiza kuanzia leo Machi 30, 2022 hadi ifikapo  Aprili 30, 2022 watoto hao wawe wamepelekwa kuanza masomo na wazazi watakao kahidi agizo hilo tutawachukulia hatua kali” amesema Mwenda.

Akizungumzia ukaguzi wa miradi hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh.9  Bilioni amesema kamati hizo zilifanya ukaguzi huo ili kuona nini kimefanyika katika mwaka mmoja wa uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi  kwa ajili ya kutekeleza miradi katika Tarafa hiyo ambapo waliridhishwa na utekelezwaji wake.

Alisema  Serikali inatumia fedha nyingi kuitekeleza akitolea mfano ujenzi wa madarasa yaliyotokana kwa fedha za mradi wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 ambayo yamewaondolea adha kubwa ya michango wananchi ya kuchangia ujenzi na ununuaji wa madawati.

Aidha Mwenda aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vijana wanaoshiriki katika zoezi la anuani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima kwa kuwaelekeza majina ya mitaa na mambo mengine yanayohitajika na akawaomba kufanya hivyo pia katika zoezi la Sensa ya watu na makazi.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi aliwaomba wakandarasi waliopewa kuijenga miradi hiyo kuijenga kwa wakati kama walivyo kubaliana kwenye mikataba ili wananchi waweze kuanza kuitumia kwa wakati.