Nuru FM

Machi 28, 2022 wapangaji wanunuzi kuhamia

26 March 2022, 6:54 am

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) imefanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 23 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota juu ya wakazi hao kununua nyumba hizo kwa utaratibu wa mpangaji- mnunuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika nyumba za makazi Magomeni Kota jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Said Mndeme amesema katika utekelezaji wa maagizo hayo wamefanya ukokotozi wa gharama hizo na kukamilisha ambapo taratibu zinazofuata ni za kiserikali ikiwemo kupata vibali na baadaye gharama hizo kutolewa kwa wahusika.

Mndeme amesema, zoezi hilo halitaathiri taratibu za makabidhiano na kuanza kwa matumizi ya nyumba hizo na mchakato wa makabidhiano hayo utaanza Jumatatu Machi 28, 2022 kwa wakazi 144 ambao wamepangwa katika ratiba wataanza mchakato wa kuhamia katika makazi hayo

“Tayari tumeweka utaratibu mzuri wa kuhamia kwa wakazi wa hapa si kwa kupewa funguo… Kutakuwa taratibu za makabidhiano kuna fomu maalum zinazohusisha hali zote za nyumba na baada ya wakazi kuzikagua na kuridhika watasaini na maafisa wa TBA pia watasaini na watapewa pia barua za ofa zinazoonesha wamepewa nyumba hizi kwa utaratibu wa mpangaji-mnunuzi.” Amesema Mkurugenzi Mndeme

Amesema kuwa, watakuwa na ofisini hapo katika kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa haraka na wakazi watarajiwa wanakabidhiwa nyumba hizo kwa wakati.

Aidha kuhusiana na utunzaji wa mradi huo Mndeme amesema Kutakuwa na na wataalam wa umeme na mabomba wakati wote pamoja na wafanyakazi wa idara ya Miliki kutoka Wakala hiyo watakaokuwa wanasimamia nyumba hizo.