Nuru FM

DC MOYO: Kurejeshwa Mahakama Kata Ya Maboga Hakutoathiri Shughuli Za Mahakama Ya Ifunda

25 March 2022, 9:05 am

Mkuu Wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amewakikishia Wakazi Wa Tarafa ya Kiponzero kuwa kurejeshwa Kwa shughuli za kimahakama katika Kata ya Maboga hakutoathiri shughuli za kimahakama zinazoendelea kata ya Ifunda.

Akizungumza na viongozi wa vijiji na kata za Tarafa ya Kiponzero Mkuu wa Wilaya huyo alisema kuwa alipata malalamiko ya kuhamishwa kwa mahakama kutoka Kiponzero kwenda Ifunda jambo ambalo limenipelekea kulifanyia kazi suala hilo kushirikiana na mamlaka husika.

Alisema kuwa mahakama ya mwanzo Kiponzero itarudi na kufanya kazi zake katika kijiji cha kiponzero kama ambapo ilikuwa awali na kuwahudumia wananchi wote wa Tarafa ya Kiponzero

Moyo alisema kuwa  kilichobakia ni makubaliano ya wananchi kuanza kuchangia ujenzi wa choo na kukarabati jingo la mahakama ambapo kinatakiwa kiasi cha shilingi milioni sita (6,000,000)

Alisema kuwa viongozi wa vijiji vyote kumi na tano wamekubali kuchangia kiasi cha shilingi lakini nne (400,000) na mwisho wa michango ya wananchi ni tarehe 30/4/2022 ili zoezi la ukarabati na ujenzi wa choo uanze mara moja.

Moyo alisema kuwa Mahakama iliyopo Ifunda itaendelea na shughuli zake Wakati huo huo Mahakama ya mwanzo ya Kiponzero pia itakuwa ikitoa huduma kwa lengo la kusaidia wananchi kupata huduma za kimahakama kwa urahisi zaidi.

Alisema kuwa Tarafa ya Kiponzero inajiografia ngumu kidogo hivyo serikali imeamua kuwa wananchi ambao wapo karibu na mahakama ya Ifunda wataendelea kupata huduma za kimahakama Ifunda hivyo hivyo na wananchi waliopo karibu na kijiji cha Kiponzero nao watapata huduma hiyo.

katika kikao hicho viongozi wa Tarafa hiyo wamekubaliana Kwa pamoja Ili kufanikisha Ukarabati wa jengo la Mahakama ya Kiponzero Wananchi watachangia kiasi cha shilingi milioni sita na kinachosalia kitatolewa idara ya mahakama.

Aidha mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa ametembelea ujenzi wa ofisi ya Afisa Tarafa ya Kiponzero na ujenzi unaendelea vizuri na hivi karibuni ofisi hiyo itaanza kufanya kazi.

Moyo alisema kuwa baada ya wiki mbili wananchi wa Tarafa ya Kiponzero wataanza kupata huduma kutoka kwa Afisa Tarafa katika makao makuu ya Tarafa hiyo katika kijiji cha Kiponzero.

Aliwaomba wananchi kumuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan ili aweze kuwaletea maendeleo na huduma zote muhimu karibu na wananchi.

Nao baadhi ya wenyeviti na watendaji wa vijiji,kata na Tarafa hiyo wamesema kuwa wamefurahishwa na kitendo cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan kuamua kuwasogezea huduma ya kimahakama karibu yao.

Walisema kuwa kulingana na ukubwa wa Tarafa hiyo kulikuwa kunawatesa baadhi ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kimahakama ili kupata haki zao ambazo wanakuwa wanazidai kisheria.

Amina said ni m kazi wa kijiji cha Maboga alisema kuwa wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi kwa kuwa mahakama ilikuwa mbali na maeneo yao kiasi kwamba kesi nyingi walishindwa kuzifaatili kutokana na kutumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo.