Nuru FM

Siku 365 Za Mheshimiwa Rais Samia Zaweka Alama Ya Mafanikio Makubwa Katika Sekta Ya Masoko Ya Mitaji

24 March 2022, 6:00 am

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji katika kipindi cha siku 365 za uongozi wake.

Akielezea mafanikio makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema, mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi bora na madhubuti wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bw, Mkama ameongeza kuwa uchumi wa kidiplomasia na ziara za Rais nje ya nchi zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kuvutia wawekezaji toka nje ya nchi na kuleta mafanikio zaidi katika masoko ya mitaji.

Bw. Mkama amesema, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja n· Thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 12.02 na kufikia shilingi trilioni 32.67 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 29.16 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

Amesema kuwa Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 19.2 na kufikia shilingi trilioni 3.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.6 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

Ameongeza kuwa Mauzo ya hatifungani za Serikali yameongezeka kwa asilimia 38.1 na kufikia shilingi trilioni 2.9 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

Hata hivyo amebainisha kuwa  Thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja katika kipindi kilichoishia Februari 2022 imeongezeka kwa asilimia 55.8 na kufikia shilingi bilioni 868.51 ikilinganishwa na shilingi bilioni 557.28 katika kipindi kilichoishia Februari 2021.