Nuru FM

Balozi wa Utalii Nchini Isabela agusa maisha ya walemavu watatu wa familia moja Mkoani Iringa

21 March 2022, 5:36 pm

Familia ya watu watatu wenye ulemavu wa Viungo Katika Kijiji cha Lulanzi kilichopo Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa wamekabidhiwa msaada wa Mahitaji ya Kibinadamu na Balozi wa Utalii Tanzania Bi Isabela Mwampamba.

Msaada waliopewa ni pamoja na Mchele, mafuta ya kupikia, nguo, blanket, mafuta ya kupaka na mahitaji mengine muhimu kwao.

Akizungumza mara baada ya kupokea Msaada huo, Mama Mzazi wa walemavu hao watatu, Bi Angelis Mwandigali Mwenye Umri wa Miaka zaidi ya 70 ameshukuru kwa kupewa msaada wa vitu hivyo kutoka kwa Balozi Isabela akiongozana na kundi la wanawake watalii wa nyanda za juu kusini.

Amesema kuwa Isabela amekuwa msaada kwao toka mwaka 2018 kwa kuwapatia msaada wa mahitaji mbalimbali jambo lililopelekea aweze kuwalea watoto wake hao ambao mkubwa ana miaka 48 na wengine wana miaka 42 na watatu ana miaka 40 na wamekuwa katika hali hiyo Toka walipokuwa wadogo.

Hata hivyo Mama mzazi wa Watoto hao ambaye ni Mjane kwa sasa  amemuomba, Bi isabela na kundi la wanawake wenzake waliofika kutoa msaada huo kuwasaidia kujenga  jiko na sehemu ya kuwapumzisha watoto wake pindi wanapohitaji kukaa nje.

Akizungumza huku akibugujikwa na machozi wakati wa kukabidhi msaada huo Bi isabela Mwampamba amesema kuwa ameendelea kuisaidia familia hiyo kwa kutoa fedha kutoka katika Taasisi yake toka mwaka 2018 kwa kuwatumia mahitaji huku akiwashukuru wanawake wenzake kwa kushiriki katika tukio hilo.

Bi Isabella amesema kuwa baada ya kupata changamoto hiyo wameamua kuanzisha kikundi cha wanawake ambacho tayari kimeanza kukusanya fedha kwa ajili ya kuanza kutatua baadhi ya changamoto ikiwemo ya maji na kukarabati jiko huku akiwaomba wadau wengine na serikali kuwasaidia walemavu hao.

Kwa upande wake Hoza Mbura kutoka Bodi ya Utalii  Kanda ya Iringa ameahidi kulikarabati jiko ambalo limeanguka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Kijiji hicho.

Balozi wa Utalii Bi. Isabella Mwampamba Yupo Mkoani Iringa, akiwa na wanawake ambao ni wadau wa utalii Nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na wizara ya utalii kupitia bodi ya utalii kanda ya iringa wameamua kufanya utalii wa kutembelea vivutio vilivyopo Mkoani Iringa sambamba na kuikumbuka jamii kwa kutoa misaada.