Nuru FM

Serikali yapokea vifaa tiba kutoka Ufaransa

15 March 2022, 7:51 am

Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali ya Ufaransa, kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Liberata Mulamula, ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa Msaada huo na kusema vitasaidia katika mapambano dhidi ya Uviko -19.

Amesema kwamba, msaada huo ni ishara ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ufaransa, huku akibainisha kwamba Ufaransa imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo katika nyanja mbalimbali mathalani, elimu, miundombinu, nishati na afya

Naye, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha uhusiano baina ya nchi ya Tanzania na nchi nyingine jambo linaloleta fursa za kimaendeleo nchini katika Sekta mbalimbali, hususan Sekta ya afya.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Mhe.Nabil Hajlaoui amesema Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, kwani nchi hizi mbili zimekua na mahusiano mazuri ya muda mrefu.

Sambamba na hilo Balozi Mulamula amepokea msaada wa dawa za albendazole zenye thamani ya shilingi Milioni 550 ikiwa ni ongezeko la dawa zenye thamani ya shilingi Milioni 340 zilizotolewa mwezi Februari, 2022.

Aidha, Mhe. Balozi Mulamula amewashukuru Shirika la World Vision Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya ili wananchi wapate huduma bora.

Akitoa msaada huo, Mkurugenzi wa Shirika la World Vision Tanzania Dkt. Diana Mndeme amepongeza Jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na kuweka wazi kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za afya, hasa afya za watoto.