Nuru FM

Dc Moyo apongeza juhudi za Dr Mgao kufungua Kituo cha Afya Ihomasa

4 September 2021, 5:31 pm

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amempongeza  Dr. Adelitus Basil Mgao kwa kuamua kuwekeza na katika sekta ya afya na kufungua kituo cha afya katika Kijiji cha Ihomasa Kilichopo Kata ya Wasa Wilaya ya Iringa.

Mh. Moyo ametoa kauli hiyo mara baada ya kufanya ziara katika kituo hicho cha afya ambacho kitaitwa Dr. Mgao Health Center na kuongeza kuwa Mwekezaji huyo amekuwa mfano wa kuigwa kwa kuamua kurejea kwao na kutatua changamoto ya afya ambayo iko kwa muda mrefu katika kijiji hicho.

Aidha Dc Moyo amebainisha kuwa uwepo wa kituo hicho cha afya utasaidia wananchi wa kupata huduma za afya huku akiwataka wananchi wa kata ya wasa kutunza kituo hicho ambacho ni kikubwa na cha kisasa.

“Kwa kweli nimpongeze sana mwekezaji huyu kwa kufanya uwekezaji wa kujenga kituo cha afya na kuamua kutatua changamoto ya afya katika Tarafa ya Kiponzelo Kata ya Wasa, kwa hiyo ni jambo la kuungwa mkono kwani nina imani vifaa tiba na huduma za afya zote zitapatikana hapa” amesema Dc Moyo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa ameridhishwa na ubora wa majengo na mzingira ya kituo hicho cha afya ambacho kinatarajiwa kuanza kuwahudumia wananchi kuanzia miezi mitatu ijayo.

“Kwa kweli majengo yanaridhidha na mazingira yako vizuri na pia nafurahishwa na uwepo wa kifaa cha kuchomea taka, pia nimpongeze kwa kuamua kuwajengea watumishi wake kwa sababu watakuwa katika eneo la kazi na hivyo kuwahudumia wananchi, sisi tunamtakia kila la heri” alisema Mkuu huyo wa Wilaya

Alisema kuwa serikali itashirikiana na Mwekezaji huyo huku akimuahidi kuhakikisha atapata huduma zote ikiwemo maji na umeme pindi atakapoanza kutuma maombi serikalini ili aweze kuwahudumia wananchi kwa muda muafaka.

Kwa upande wake Mwekezaji wa Kituo hicho Dr. Adelitus Basil Mgao amesema kuwa ameamua kuwekeza katika Kijiji cha Ihomasa kata ya wasa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ambazo wanazifuata mbali katika kituo cha afya cha Kiponzelo.

Dr. Mgao amesema kuwa katika kituo chake cha afya watatoa huduma zote za afya kwani kuna kila idara na huduma zitaanza kutolewa huku akitarajia kukamilisha ujenzi wa nyumba za watumishi.

“Nimeamua kuleta huduma afya karibu na wananchi ili kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi na pia nimeamua kuisaidia serikali kuhakikisha kituo cha afya kinakuwepo katika kata ya hii na huduma zitaanza kutolewa kuanzia mwezi wa 12 mwaka huu” amesema Dr. Mgao