Mpanda FM

CHADEMA na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi

26 May 2023, 10:26 am

KATAVI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kitaendelea kusimamia misingi ya chama hicho kwa kutetea haki, uhuru, na demokrasia kwa wanachama wa chama hicho na wananchi wa taifa kwa ujumla.

Akiwahutubia wanachama wa chama hicho katika uzinduzi wa Oparesheni 255 katika mkoa wa Katavi kwenye viwanja vya shule ya msingi Kashato chenye lengo la kufikisha ujumbe kwa wanachama kuhusu takwa la Katiba Mpya, mwenyekiti wa chama hicho taifa Freeman Mbowe amesema kuwa chama hicho kinahitaji Katiba Mpya kwa kuwa ni hitaji lao kwa suluhu ya changamoto mbalimbali.

Ameeleza kuwa chama hicho kitaendelea kuamini katika misingi hiyo ili kuweza kufikia malengo yake ya kushika dola kwa kuwa chama hicho bado kimebakia kuwa tumaini la watanzania katika kuleta mabadiliko ya kweli.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara Tundu Lissu amesema kuwa takwa kubwa la chama hicho ni Katiba Mpya ambayo itaondoa urasimu na ubadhirifu wa mali za umma unaojitokeza kwa sasa.

Katibu Mkuu wa chama hicho taifa John Mnyika amesema kuwa kwa muda sasa kumeshuhudiwa kuporomoka kwa sekta ya kilimo kutoka asilimia 4.9 mpaka 3.9 hali hiyo ikisababisha maisha ya vijijini kuwa magumu.

Oparesheni hiyo ya 255 itadumu kwa muda wa siku tatu katika mkoa wa Katavi kwa kutembelea majimbo ya mkoa wa Katavi kwa lengo la kuangalia uhai wa chama na kupeleka ujumbe juu ya umuhimu kuhusu Katiba Mpya.

#mpandaradiofm97.0

#chadema

#ccm