Mkoani FM

KISWAHILI: FURSA YA UKOMBOZI WA KIUCHUMI KWA WANAWAKE KUFIKIA UONGOZI

24 February 2023, 6:43 am

 

NA KHADIJA RASHID, PEMBA

“Kiswahili kimenifanya niwe maarufu ndani na nje ya nchi kwani nilikipenda tangu nipo skuli”

“Licha ya kuwa maarufu nchi mbali mbali lakini pia tunapata maendeleo binafsi pamoja na kwenye nchi zetu”

Si kauli ya mtu mwengine bali ni ya Dk. Consalata Peter Mushi Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Tanzania.

Kwa sasa mwanadada huyo kwake Kiswahili kimekua kama chanda na pete, kwani hawezi kukikosa kutokana na mafanikio aliyojipatia.

Anasema Dk. Consalata kuwa, ameanza kuipenda lugha ya Kiswahili tangu akiwa skuli ya msingi na kwa sasa anafaidi matunda kwani anatembea maeneo tofauti kutona na umaarufu alioupata kupitia lugha hiyo.

‘Penye Nia Pana Njia’ ni msemo wa Kiswahili ambao aliutumia Dkt.Consalata kwani sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ambapo anafanya kazi kwa kwa bidii ili kuhakikisha anapata mafanikio zaidi.

Sio Dk. Consalata tu aliejipatia mafanikio kutokana na lugha ya kiswali bali kuna Diana Rose Oyuka ambae ni raia wa Kenya anasema kiswali kinampaisha mithili ya ungo wa kichawi unaopaa angani nyakati za usiku.

Anasema, licha ya changamoto na vikwazo alivyowahi kupitia, lakini alionesha ujasiri kwa vile anaipenda, kiasi kwamba sasa amesahau machungu aliyopitia.

“Licha ya kuwa mwalimu katika skuli maalum ya wasichana ninaefundisha  lugha ya Kiswahili, lakini pia lugha hii inaniwezesha kufika nchi tofauti ambazo sikutegemea kufika, ikiwemo Tanzania hususan kwenye visiwa vya marashi ya karafuu na nimefika”, anaeleza.

Kauthar Is-hak kutoka kisiwani Pemba nae anaendelea kujenga umaarufu mkubwa katika nchi tofauti duniani na amewahi kuwa ‘MC’ kwenye Kongamano la Kiswahili huko Wonshgtone nchini Marekani.

“ Kupewa jina la ‘Mc’ Balozi Kauthar, hiki ni kitu cha kujivunia sana, hata hivyo pia nimebadilisha hali ya uchumi wangu kupitia lugha yetu ya Kiswahili, jambo ambalo linanipa faraja zaidi”, anasema MC huyo

Saade Said Mbarouk ambae ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) anasema, Kiswahili kwake kimekua sawa na maji, kwani anapokikosa hujiona maisha yake yapo hatarini.

Kimesababisha maisha yake kubadilika na kuonekana angavu mithili ya mbara mwezi na ndio maana anajivunia sana lugha ya kiswahili.

“Nilifundisha sana nikiwa mwalimu wa kawaida katika skuli tofauti za Unguja lakini baada ya kumaliza Shahada yangu ya Uzamili (Master) niliogolea kwenye bahari ya Kiswahili kwa kuchaguliwa kushika nafasi hii ya Mwenyekiti”, anafahamisha.

Kina mama wengi wamejisajili kwenye kanzi data kufundisha ukalimani, kuandika vitabu na wengine wanafanya kazi za tafsiri na hata waandishi wa habari wanakitumia Kiswahili kwenye kuhabarisha, kuelimisha na kukosoa kupitia vipindi vyao, ambapo lengo lao ni kukikuza Kiswahili.

Sasa Kiswahili kimekua lulu kwa wanawake wengi kwani wamebadilisha mitazamo na kujua Kiswahili ni Ng’ombe walio nona katika kipindi cha ukame.

“Kwa sasa nchi ya Tanzania Kiswahili imekua ni fursa hasa kwa wanawake kujikomboa kiuchumi na  kushiriki katika ngazi za maamuzi” anendelea kueleza.

HARAKATI ZA KUANZA KUSAMBAZA KISWAHILI NJE YA NCHI

Kupitia Bakiza aliweza kusambaza Kiswahili sanifu na fasaha ndani ya Tanzania na nje ya nchi hii akiamini ni fursa hasa kwa wanawake kwa vile wengi ni waalimu wa somo hilo kwa skuli za msingi na sekondari.

“Nimefika mpaka nchini Uholanzi, Abudhabi na Burundi kwa kusambaza lugha ya kiswahili lakini pia nimeweza kubadisha maisha yangu binafsi kwa kiwango kikubwa Kiswahili kwani namudu maisha yangu na ndugu zangu kupitia lugha hii pia kimeniinua kiuchumi” anasema Consalata.

Dr. Mwanahija katibu mtendaji BAKIZA,kwake pia Kiswahili ni sawa na chakula cha sikukiasi ya kwamba haiwezi kupitasiku bila kukitumia kuongeza ubunifu na ufanisi a kazi zake.

“Kiswahili kimesaidia kwa kiasi kibuwa kwani hata nafasi niliyonayo kwa sasa ni msaada a kuijualungha ya Kiswahili” alisema Dkt. mwanahija.

“Vilevile Kiswahili kimenisaidia kujuana na watu wengi sambamba na kutembea mikoa tofauti nchini Tanzania na njeya nchi za afrika mashariki kama vileafrika ya kusini, hali iliyoniongezea umahiri katika kazi zangu na kunifanya kuwa mdau mkubwa katika kueneza kiswahili najivunia sana.”aliongeza Dkt.Mwanahija.

NCHI ZILIZOFANIKIWA KUPITIA KISWAHILI

Ukitoa nchini Tanzania ambapo lugha ya Kiswahili ndio lugha rasmi na lugha mama, lakini zipo nchi ambazo zinafanikiwa na kupiga hatua kimaendeleo kwa lugha hiyo.

Nchini Kenya kwa miaka kadhaa Kiswahili kimekumbwa na changamoto kwani walitumia zaidi lugha ya kiingereza kuliko kiswahili, ingawa nchini humo lugha hiyo ni Rasmi na ya utaifa

Ila kwa sasa wameamka na kuwa skuli maalum ya kufundisha lugha hiyo hali inayosaidia katika kukua kwa uchumi wa nchi hiyo kwani wanawake wanaanza kujiajiri, mfano nzuri ni huyo Diana Rose Oyuka.

Kwani Diana anafundisha lugha hiyo kwa wageni wanaotoka Marekani, Sudan na Uswis hali iliyomfanya awe maaarufu zaidi na kushika nafasi ya Ujumbe kwenye Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) na Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA)”.

Kiswahili nchini Kenya na Tanzania hutumia kama lugha Rasmi, Sanifu, ya Uzawa na Lugha ya Kitaifa.

Ikiwa kwa nchi nyengine kadhaa za Afrika ya Mashariki lugha hiyo inatambulika kama Sanifu, Rasmi na lugha ya Kimataifa.

Ni dhahiri kwamba lugha ya Kiswahili inaendelea kupata umaarufu wa kufundishwa Afrika kote na Ughaibuni.

Nchini Marekani Kiswahili hutumika kuleta maendeleo kutoka nchi za Ulaya, China na hata za Afrika Mashariki, kwani hufundishwa watoto wao lugha hiyo, ili kuwa wafanyabiashara na viongozi wa baadae lengo kuongeza kipato.

Niliyajua hayo baada ya kukaa na Dk, Mahiri Mwita kwa takribani dakika 10 ambae ni mwalimu wa Kiswahili nchini humo.

Pia alinieleza kuwa, ni vyema kwa Tanzania sasa kuamka na kukitumia Kiswahili ili kujipatia maendeleo na sio kusubri na kujinata kwa kusema lugha hiyo ni ya kwetu, ililhali hatuoneshi kuitendea kazi.

“Watanzania walio wengi wakihaha huku na kule kujifunza lugha za kigeni wakiamini ndio zinaweza kuwatoa kimaisha, lakini kwetu Marekani tunaipigania lugha ya Kiswahili kama ni chachu ya maendeleo”, alisema Dkt. Mahiri.

Nako  nchini Uganda, Kampala  mwalimu Kato Herbert anaefundisha katika skuli ya wanawake , ambapo baada ya mazungumzo ya dakika 5 ya kutimbwishana kwa lugha yangu ya uzawa alitoa ushuhuda wa wanafunzi wake kwa vile hawajawahi kushika mkia kwenye lugha hiyo.

“Nafundisha lugha ya Kiswahili katika skuli ya wanawake nchini Uganda ila wanakua na mori ya kujifunza hali inayoniongeza ari ya mimi mwalimu kwani wanajuhudi za vitendo zaidi”alisema Kato.

Mwamwingila Goima Mwamwingila mtunzi na mwandishi wa vitabu Kutoka Mtalimbo Books anayesanifisha mawazo kupitia lugha hiyo, kwani hubadilisha udongo kuwa almasi.

“Nani shuhuda wa maendeleo ya wanawake kupitia luga ya Kiswahili, Lakini pia tunajionea vitabu vingi vikiandikwa kwa lugha angavu na nyororo na hawa hawa wanawake, lugaha ambazo zinakurejesha kuiona Zanzibar yenye mandhari ya kuvutia ndio kwanza watu wameshika silaha kumuondosha mkoloni”, Alisema Mwamwingila

Walimu wataalamu wa Kiswahili katika Baraza la Kiswahili Tanzania ni 2,609, ambapo wanawake ni 1,478 huku Baraza la Kiswahili Zanzibar ni 637 ikiwa wanawake 453.

Mbali na kuwa lugha hiyo inafundishwa na kuzungumzwa na watu kutoka mataifa mbali mbali hivi karibuni ilitambuliwa zaidi kimataifa na Shirika la Elimu ya Sayansi na Utamaduni, UNESCO na kuwekewa siku yake ya kuadhimishwa duniani kote, ambayo ni Julai 7 ya kila mwaka, jambo ambalo ni heshima kubwa kwa lugha hiyo.

Kwani matamasha mengi huandaliwa na hutumika lugha moja tu ya Kiswahili na kuburudisha kiasi ya kumfanya msikilizaji asijihisi mchovu , huku ikikusanya vitu vyenye asili na ladha ya Kiswahili.

                                                     MWISHO.