Mkoani FM

RAISI WA ZANZIBAR:URITHI WA MTOTO NI ELIMU.

2 January 2023, 1:32 pm

RAISi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akifungua Skuli ya Mwambe Wilaya ya Mkoani.

RAISi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wanachi kusimamia fursa za elimu kwa watoto wao kwani ndio urithi mzuri wa taifa kiujumla.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo Mwambe Wilaya ya Mkoani Pemba, wakati akizungumza na wanafunzi na wananchi  mara baada ya kuifungua skuli mpya ya ghorofa mbili ya msingi Mwambe, , ikiwa ni shamra shamra za miaka 59, ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Ameeleza kabla ya mapinduzi ya Zanzibar ni maeneo machache tu ndio yalikuwa na skuli, lakini baada ya mapinduzi serikali imezingatia usawa wa elimu ili kuhakikisha  watoto wote wa Zanzibar wanapata elimu mjini na vijijini kwani elimu ndio msingi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuyaenzi na kuyatunza madarasa hayo kwani ndio yatakayofanya uwepo wa maendeleo kwa watoto wao.

Amesema kielelezo cha juhudi ya serikali katika kuimarisha sekta ya elimu ni kukabiliana na changamoto za uhaba wa madarasa ili kuepusha msongamano wa wanafunzi.

Aidha katika kuhakikisha changamoto ya walimu inamalizika ameiagiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kushirikiana kwa karibu na Idara ya Utumishi, ili kupunguza uhaba wa waalimu maskulini.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa, amesema jitihada anazochukuz rais wa Zanzibar katika sekta ya elimu ni kubwa na watahakikisha wanashirikiana na walimu na wazazi kuunga mkono jitihada hizo kwa lengo la kukuza sekta ya elimu.