Micheweni FM

Changamoto za maisha isiwe chanzo cha utoro mashuleni

14 September 2023, 9:04 am

Baadhi ya watoto katika shehia ya Tumbe wakiendesha mtumbwi (Picha na Mwiaba Kombo)

Wilaya ya Micheweni ni miongoni mwa wilaya ambazo zinaendelea kufanya vizuri katika mitihani yake ya taifa lakini bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wazazi na walezi kutowapa kipaombele watoto wao kuhudhiria skuli.

Na Mwiaba Kombo

Wanafunzi wa skuli za Micheweni kisiwani Pemba, wametakiwa kuacha utoro na kuhudhuria masomoni kikamilifu, na kuacha kisingizio cha  hali ngumu ya maisha inayowakabili.

Kauli imetolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya hiyo, Rishad Kombo Faki, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake Micheweni, juu ya utoro ambao umeendelea kukithiri licha ya serikali kuingilia kati suala hilo

Amesema hali ya kimazingira iliyopo Micheweni, isiwe chanzo kwa wanafunzi hao kukatisha masomo yao, kwani elimu ni haki yao ya msingi.

Aidha meeleza kuwa, wazazi wamekuwa wakipambana, ili kuhakikisha wanawapatia watoto wao huduma za kila siku na za lazima, hivyo ni wajibu kwa wanafunzi hao kuthamini jambo hilo.

Akizungumzia athari ya wanafunzi kuwa watoro masomoni, amesema mojawapo ni kudumaa kiakili, kuongezeka kwawasiojua kusoma na kuandika na kujirahisishia kuingia katika vitendo viovu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli ya sekondari ya Tumbe Nassor Rashid Said amesema, muamko mdogo kwa baadhi ya wazazi na walezi juu ya elimu, unasababisha kwa wanafunzi kua watoro masomoni.

Mwalimu mkuu huyo amewataka wazazi na walezi, kuwa na ushirikiano katika kuwalea vijana wao na asiachiwe mzazi wa wakike pekee, kwani kufanya hivyo, kutaporomosha maendeleo ya elimu ya mtoto.

Nao wazazi na walezi katika wilaya hiyo wamesema changamoto za maisha ndio zinazopelekea utoro kwa wanafunzi hao jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo.

Wanafunzi Sada Ali Hamad na Kombo Mohamed Said wa kidato cha pili skuli ya Tumbe, wamewawataka wanafunzi wenzao, kutojihusisha na utoro, kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha, kwani kufanya hivyo kutapoteza ndoto zao za maisha.

Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, amezitaka kamati za skuli,  wazazi na walezi, kusimamia utoro kwa wanafunzi ili kuhudhuria masomoni.