Micheweni FM

BARAZA LA HABARI TANZANIA (MCT) LAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI PEMBA KUHUSU SHERIA ZA HABARI

24 June 2022, 7:22 am

NA MWIABA KOMBO.

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kusoma na kuzielewa sheria zote, ili kufanya kazi ya habari kwa ufanisi na bila vikwazo.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu sheria ya habari   amesema,  kujua na kuzielewa sheria za habari ni muhimu sana kwa wanahabari kwani wanazitumia katika kazi zao za kila siku.

Amesema kuwa, sera, kanuni, sheria na maadili ndio yanayojenga ustawi wa habari, hivyo kuna haja kwa waandishi kuwa na juhudi ya kuzisoma sheria kila siku ili kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuepuka vikwazo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga alisema, waandishi wa habari wasipozielewa sheria, mchakato wa kupitisha sheria utakuwa kwenye mikono ya wanasheria na wanasiasa tu, hivyo wao watakuwa hawana nafasi.

Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau amwaomba waandishi wa habari kuwa makini wanapopewa mafunzo, kwani yanawajenga zaidi katika kufanya kazi zao za kila siku.

Afisa Mdhamini MCT Zanzibar Shifaa Said Hassan alifahamisha kuwa, kada ya habari ndio inayoleta maendeo katika nchi yeyote duniani, hivyo amewataka waandishi wa habari kuzidisha mashirikiano katika kukuza na kuendeleza tasnia hiyo.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Afisa huyo alisema, kuna madhila mengi yanayowakumba wanahabari ingawa wengine wanashindwa kuripoti, ambapo aliwataka waripoti MCT kwa ajili ya kurikodiwa kwenye kanzidata.

Akiwasilisha mada ya Uhuru wa maoni mwanasheria Mpale Mpoki alisema ili nchi ipate maendeleo, kuwepo kwa demokrasia na Utawala Bora lazima watu watoe waliyonayo, kwani hujenga ustawi bora wa maisha.

Mafunzo hayo ya siku moja ya sheria ya habari, yalifanyika katika Ukumbi wa Samael Gombani Chake Chake.