Micheweni FM

Mganga Pemba aliyembaka mke, ili amtoe mume wake rumande afungwa miaka 30

25 October 2021, 6:52 am

PICHA IKIONYESHA MFUNGWA ALIEFUNGWA GEREZANI.

Na Mwiaba Kombo.

MAHAKAMA ya Mkoa Chake Chake, imemuhukumu mganga wa kienyeji kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 30 na kumlipa muathiriwa fidia ya shilingi milioni 1, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mke wa rafiki yake.

Kisa cha mganga huyo, kabla ya kufanya unyama huo, alimtaka mteja wake ambae ni mwanamke, kumpatia nywele za siri na mbegu za kiume, ili afanikishe uganga wake wa kumtoa rumande mume wake.

Awali mganga huyo, alikuwa rumande kwa tuhuma za wizi huku mume wa mwanamke huyo, nae akiwa rumande kwa kosa jengine.

Ndio baada ya mganga huyo kupata dhamana, na kumuacha rumande rafiki yake ambae ni mume wa mteja wake, alimuelezea amtafutie nywele za sehemu za siri na mbegu za kiume, ili afanikishe dawa ya kumtoa rumande.

“Ili mume wako atoke rumande, wewe nitafutie vitu hivyo viwili, ambavyo vilimshinda na kumlazimisha kufanya nae mapenzi, jambo ambalo ni kosa kisheria,’’ilieleza hati ya mashtaka.

Mganga huyo aliejulikana kwa jina Issa Abdalla Haji mwenye umri wa miaka 41 mkaazi wa Wawi Chake Chake, amehukumiwa kifungo hicho mara tu baada ya kukubali kosa hilo.

Akisomewa shitaka lake na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Ali Amour Makame, mshitakiwa huyo amekubali kutenda kosa hilo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu.

Hakimu wa Mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, baada ya mshitakiwa kukubali kosa lake kwa mara ya kwanza kufika mahakamani hapo Oktoba, 19 mwaka huu, alimuamuru kwenda chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 30 na kumlipa muathiriwa fidia ya shilingi milioni 1.

Kwa mujibu wa maelezo ya hakimu huyo, mshitakiwa alikuwa rumande na rafiki yake, ikiwa yeye anakabiliwa na tuhuma za wizi, huku rafiki yake akikabiliwa na tuhuma za wizi wa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ya mshitakiwa huyo ametenda kosa hilo Oktoba 11 mwaka huu saa 12:00 jioni Wawi Chake Chake, bila ya halali alimbaka mwanamke baada ya kumuaminisha kwamba atamfanyia dawa ya kumtoa mume wake ambae yupo rumande.

Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108(1), (3), (d), na 109(1) sheria ya adhabu, sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.

Hii ni kesi ya kwanza kuwahi kutokea katika muongo mmoja sasa, kwa mshitakiwa kufikishwa mahakamani ka mara ya kwanza kukubali kosa na kisha kuhukumiwa siku hiyo hiyo.