Mazingira FM

Dkt Naano: wanafunzi 234 Jimbo la mwibara Wilayani Bunda hawajaripoti shule kuanza kidato Cha kwanza

14 February 2023, 7:18 pm

Dkt Vicent Naano Mkuu wa Wilaya ya Bunda

Jumla ya wanafunzi 234 waliofaulu kujiunga na masomo ya sekondari jimbo la Mwibara Halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara hawajaripoti shule mpaka sasa.

Hayo yamebainika leo katika ziara ya kikazi ya mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Vicent Naano iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi katika kata mbalimbali.

Kutokana na idadi hiyo imemlazimu mkuu huyo kutoa maelekezo kwa watendaji wa kata na mkuu wa kituo cha polisi Bunda OCD kuwakamata wazazi wote walioshindwa kupeleka watoto wao kujiunga na masomo ya sekondari huku akiweka msisitizo kuwa kusomesha mtoto ni lazima nasio hiari.

Wananchi Jimbo la Mwibara wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe Dkt Vicent Naano.

Katika hatua nyingine amewahimiza wazazi kuchangia chakula cha watoto shuleni kwani utaratibu huo ni maagizo ya serikali na atakaye kataa kuchangia chakula atachukuliwa hatua za kisheria.

By Theresia Thomas