Mazingira FM

Rorya: Adaiwa kuuawa na mumewe kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali

1 February 2023, 3:56 pm

Bashiri Kichere Nyitati mkazi wa Kibuyi Kata ya Nyamunga Wilaya ya Rorya Mkoani Mara anasakwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Mke wake Sesilia au Kulwa Cosmas Wang’anga kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili kutokana na wivu wa mapenzi.

Alipigiwa simu na mtuhumiwa huyo na kumwambia kuwa kama angemkuta nyumbani angeanza na yeye.

Katika tukio hilo lililotokea Jumanne tarehe 24 Jan 2023 majira ya saa 4 asubuhi mtuhumiwa alikwenda nyumbani kwao marehemu katika Kijiji cha Kyamwame kata ya Komuge Wilayani Rorya mkoani Mara na kumkuta marehemu akiwa amelala ndipo alipomshambua kwa kisu na kusababisha kifo cha mke wake huyo.

Akizungumza na Radio Mazingira Fm, Baba wa Marehemu Ndugu Cosmas Wang’anga amesema mtuhumiwa huyo alifika nyumbani na kumkuta marehemu na mdogo wake wa shule ya msingi ndipo alipoelekea moja kwa moja katika nyumba aliyekuwa amejipumzisha marehemu na kutekeleza unyama huo.

Sauti ya Cosmas Wang’anga

Kwa upande wake Mgesi Chacha Nyarubamba ambaye ni mama wa marehemu amesema wakati tukio hilo linatokea hakuwepo nyumbani lakini alipigiwa simu na mtuhumiwa huyo na kumwambia kuwa kama angemkuta nyumbani angeanza na yeye hivyo aende nyumbani aone binti yake alichomfanyia.

Sauti ya Mgesi Chacha Nyarubamba

Akizungumza wakati wa shughuli za kuaga mwili wa marehemu tarehe 25 Jan 2023 Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya akiwa ameambatana na wajumbe wengine wa kamati hiyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

Amesema katika wilaya ya Rorya tarafa ya Suba imekuwa na matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia huku wananchi wakiwa na tabia ya kuficha uhalifu na wahalifu hivyo amewataka kubadili tabia ili kutokomeza vitendo hivyo.