Mazingira FM

mgogoro kati ya wenye leseni, wachimbaji na wenye mashamaba wa Guta Stoon waanza kupatiwa ufumbuzi

14 October 2022, 4:48 pm

Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ametatua mgogoro uliokuwepo kati ya wamiliki wa mashamba, wachimbaji Wadogo na wamiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini mtaa wa Stooni Kata ya Guta halmashauri ya Mji wa Bunda.

Rc Mzee amesema kuwa baadhi ya Wananchi ambao ni wakazi wa eneo hilo wamekubaliana kufanya makubaliano na wamiliki wa leseni kwa kuzingatia Sheria na Kanuni na Taratibu za uchimbaji wa madini.

Aidha Rc Mzee amesisitiza kuwa makundi hayo yanatakiwa kuzingatia taratibu walizoziweka wenyewe kisheria na mara taratibu hizo zitakapokamilika wataruhusiwa mara moja kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini.

Pamoja na hayo Rc Mzee ameongeza kwa kusema kuwa wale wote ambao bado hawajaingia makubaliano waendelee na shughuli za ufugaji na kilimo katika maeneo yao.

Hata hivyo Rc Mzee amekemea vitendo viovu vya uvunjaji wa Sheria na amani kwa kuwashambulia Askari Polisi, Watumishi wa Umma na Viongozi wanaofika katika eneo hilo kutafuta suhulu ya matatizo yao.