Mazingira FM

Bunda: Wawili wanusurika kifo baada ya nyumba kuwaka moto usiku

July 19, 2022, 1:03 pm

Watu wawili wanusurika kifo kwa kuungua moto wa maajabu uliotokea usiku saa 8 wakiwa wamelala.

Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa kuamkia  July 18, 2022 katika mtaa wa Majengo Mapya kata ya Nyamakokoto Halmashauri ya mji wa Bunda ambapo walionusurika katika tukio hilo ni Dorica Bwire (56) na Levina Bwire (20) ambaye ni mtoto wa kaka yake

Kwa mujibu wa mashuhuda na majirani wamesema walishtushwa na sauti kali mithili ya bomu au radi jambo lililofanya waanze kupiga kalele za mwizi wakidhani wamevamiwa lakini baada ya dakika chache ndio walibaini tukio hili kwa jirani yao.

Paulo Owiti na Bi Lucy Mwita ambao ni majirani wamesema walifika katika mji huo na kukuta wawili hao wakiwa wameungua moto huku paa la chumba walichokiwa wamelala likiwa limefumuka na ukata wa nyumba hiyo ukiwa na nyufa ndipo walipotoa msaada wa kuwapeleka hospitali.

Kipeta Stephano ambaye ni kijana wa mama huyo aliyekuwa amelala chumba jirani anasema alishtushwa na sauti hiyo na ghafla alisikia sauti ya mama yake akiomba msaada ndipo alipotoka nje na kwenda kupomoa mlango na kufanikiwa kuwatoa huku mama yake akiwa ameungua sehemu za kichwani mdogo wake akiwa ameungua kuanzia kiunoni kushuka chini na mkono wa kulia.

Amesema alipoingia ndani alikuta moto unawaka kwenye godoro na neti huku wawili hao wakiwa wanatapatapa kutafuta njia ya kutoka na mara baada ya kutuliza hali hiyo ndipo walipopigwa na butwaa katika kutafakari nini chanzo cha moto huo ikiwa umeme na gesi ndani ya chumba hicho ni viko shwari.

Mazingira Fm bado iko katika juhudi za kuwasiliana na mamlaka husika kubaini nini chanzo cha moto huo ikiwa Majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu hospitali ya DDH mjini Bunda na hali zao zinaendelea vizuri.