Mazingira FM

Mhe. Mabotto: Wataalamu wa sekta ya Madini chanzo Cha migogoro kwenye migodi ya wachimbaji wadogo

June 21, 2022, 7:27 am

Mbunge wa Bunda Mjini, Robert Chacha Maboto amesema suala la wananchi kuvumbua sehemu ya uchimbaji wa madini kisha wataalamu na wasimamizi wengine kutafuta watu wanakwenda kukata leseni bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika limekuwa likileta mgogoro mkubwa.

 

Maboto ameyasema hayo leo Bungeni Dodoma wakati akichangia hotuba ya Bajeti iliyowasilishwa Bungeni na Wizara ya Fedha na Mipango wiki iliyopita.

 

Amesema suala la madini bado lina matatizo makubwa kwani wananchi wamekuwa wa kwanza kuvumbua madini katika maeneo yao na mara baada ya kuvumbua madini hayo baadhi ya wataalamu na viongozi wa wachimbaji wamekuwa wakitafuta watu wanakata leseni za maeneo hayo pasipo kuwashirikisha wananchi.

 

“Wananchi wetu kwenye maeneo yao wanayoyaishi wao ndio wanakuwa wa kwanza kuvumbua kuwa sehemu hii ndio kuna madini, wakishavumbua hawa wataalamu wetu wanachokifanya ni kwenda kutafuta watu ambao wanakwenda kukata leseni kwenye eneo lile bila kuwahusisha wananchi wenyewe wahusika” Maboto

 

Ameongeza kuwa “kiongozi wa wasimamizi wa wachimbaji wadogo wa madini nchini, yeye mwenyewe ni mfanyabiashara wa madini halafu yeye ndio anawasimamia wachimbaji wadogo halafu yeye huyo ndio akawatafute wenye mashamba kuzungumza nao nao jambo hili halijakaa vizuri”.

 

Mabato amesema kiongozi wa wachimbaji wadogo wa madini nchini anatakiwa atokane na watu ambao hawana ‘interest’ yoyote na uchimbaji wa madini ndio ataweza kuleta haki kati ya wenye mashamba, wenye leseni na wachimbaji wadogo.

 

“Anapewa mtu kusimamia wachimbaji wadogo aidha wenye mashamba na sehemu ya kuchimba madini ambayo yeye mwenyeye ‘anainterest’ na uchimbaji wa madini jambo hili linaleta migogoro mikubwa sana kwa wananchi wetu”

 

“linawafanya waone wao kama raia wa kawaida wamegundua eneo lile la uchimbaji wa madini huyu yeye kwasababu yuko ngazi ya juu anaenda kutafuta leseni anakuja kuwaambia kwamba eneo hili tulishakata leseni miaka mitano iliyopita na wakati madini labda yamevumbuliwa mwaka mmoja uliopita jambo hili linaleta mgogoro mkubwa sana kati ya wananchi na wizara ya madini”

 

Aidha Mh Maboto amesisitiza kuwa jambo hili lisipowekwa vizuri anaamini kuna siku litaleta mgogoro mkubwa kwasababu wananchi wanaona kama wananyimwa haki zao.

Kauli hii ya Maboto inakuja wakati kukiwa bado na mgogoro kati ya wenye mashamba na wenye leseni katika machimbo ya mgodi wa Kinyambwiga kata ya Guta Jimbo la Bunda Mjini ambapo shughuli za Uchimbaji katika eneo hilo zilisitishwa tangu mwezi May 2022 kwa agizo la mkuu wa Mkoa wa Mara.