Mazingira FM

Bunda; Wakulima wa pamba waomba kukopeshwa pembejeo

November 10, 2021, 8:58 pm

kiwango cha mbegu kilichoandaliwa

Baadhi ya Wakulima wa zao la pamba kata ya Kunzugu Halmashauri ya Mji wa Bunda wameiomba serikali isimamie zoezi la usambazaji wa mbegu ya pamba kwa kuwakopesha wakulima kama ilivyokuwa msimu uliopita tofauti na utaratibu wa msimu huu unaowataka walipie pesa tasrimu jambo linalowafanya washindwe kulima zao hilo.

Wakizungumza na Radio Mazingira Fm kwa nyakati tofauti ilipowatembelea katika maeneo yao hapo jana 8 Nov 2021, wamesema utaratibu unaotumika kwa sasa umewafanya baadhi yao washindwe kumudu gharama hizo na hivyo kuangalia nafasi ya kuachana na zao hilo kwa msimu huu jambo litakalopelekea kukwamisha uchumi wao na taifa kwa ujumla.

“Kulima tunapenda ila tatizo ni pesa ukipata pesa kidogo unaitumia kununua chakula na tulikuwa tumezoea kama misimu iliyopita kwamba mbegu tunakopeshwa wakati wa kuuza tunalipa kwahiyo kuigawa pesa hiyo kwa ajili ya matumizi ya chakula na mbegu tunashindwa tunaiomba serikali itusaidie tukopeshwe mbegu za pamba”alisema Shida Magesa mmoja kati ya wakulima wa pamba.

Kwa upande wake Mkulima Mwezeshaji na Katibu wa Chama Cha Ushirika AMCOS Kunzugu, Nyang’era Lukiko amesema tangu waanze zoezi la kuuza mbegu ya Pamba bado uitikio wa wakulima umekuwa ni wa kusuasua huku huku moja kati ya sababu inayotajwa ni kutokana na utaratibu uliopo unaowataka wakulima wanunue pamba kwa pesa taslimu katika vituo vya vyama vya ushirika.

mkulima mwezeshaji na katibu wa AMCOS kunzugu kituo B Nyang’era Lukiko

Nyag’era amesema tangu waanze zoezi la kuuza mbegu za pamba ambapo ni zaidi ya mwezi mmoja sasa wamekwishauza mifuko miwili tu ya mbegu ambayo ni sawa na kilo arobaini kati ya mifuko 330 ambazo ni sawa na kilo 6,600 walizopokea kutoka katika makampuni mbalimbali.

Naye Diwani wa Kata ya Kunzugu, Mh. Pasaka Shabani Samson amesema suala hilo amekwisha liwasilisha katika vikao vya Halmashauri baada ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wakulima na kuongeza kuwa kama hapatakuwa na mkakati madhubuti zao hilo litaendelea kuporomoka kwani kwa msimu uliopita liliweza kuchangia kiasi cha shilingi milioni 30 pekee wakati hapo awali lilichangia zaidi ya milioni 120 ya mapato yatokanayo na pamba.

By Edward Lucas