Mazingira FM

Apoteza maisha wakati akivuka mkondo wa maji wa ziwa Victoria

October 5, 2021, 3:01 pm

Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Dotto Mbogo au maarufu kama Mwanambogo mkazi wa Tamau kata ya Nyatwali Halmashauri ya mji wa Bunda amefariki dunia baada ya kuanguka na kufa maji katika mkondo wa mto Rubana na Ziwa Victoria.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema mwanamke huyo amekufa maji wakati akijaribu kuvuka kwa miguu katika mkondo huo ambapo kwa hali ya kawaida wenyeji hutumia mtumbwi.

Dotto Kihiri Mirumbe ambaye ni Afisa mtendaji wa mtaa wa Tamau amesema akiwa anasogea katika katika eneo hilo ili kuangalia hali ya mtumbwi ghafla alimuona mtu ng’ambo ya pili akiwa anazama.

“Kipindi nasogea ili nione hali ya mtumbwi ghafla upande wa pili wa mto nilimuona mtu akiwa anazama huku akinyoosha mkono kuomba msaada na upande huo kulikuwa na wanawake wawili ambao walishindwa kuingia majini kumtoa”

Mirumbe amesema baada ya kuona tukio hilo aliwasihi watu kupiga kelele kuomba msaada ambapo baada ya dakika kadhaa walijitokeza vijana wanne na kuingia majini ambapo walikuta tayari amefariki dunia.

George Nyerere ni Mmoja kati ya vijana waliojitosa majini amesema katika juhudi za kumtafuta kwa dakika kadhaa hatimaye alifanikiwa kumpata kando kidogo ya mto huo kwa mwanzoni kina cha mapajani akiwa amefariki dunia.

Jeshi la polisi na daktari wamefika katika eneo la tukio kuthibitisha.

By Edward Lucas