Mazingira FM

Ahofiwa kupoteza Maisha wakati akivua samaki ziwa Victoria

October 3, 2021, 11:07 am

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Lugoye Ndimila (31) mkazi wa mtaa wa Kariakoo Kata ya Nyatwali Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara anasadikiwa kufariki duniani akiwa katika shughuli za uvuvi kando ya Ziwa Victoria usiku wa kuamkia tarehe 2 Oct 2021

Akielezea tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo, Jumanne Abdallah maarufu kama Makamba amesema alipigiwa simu majira ya saa tisa usiku na mwananchi wa eneo hilo akimwelezea kuhusu tukio hilo.

Makamba anasema alifika eneo la tukio na kuelezwa kuwa mtu huyo alikuwa katika shughuli za uvuvi akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Shukurani au Shida na kila mmoja akiwa kwenye mtumbwi wake na mara ghafla Shida alimsikia mwenziye anapiga kelele ya ghafla kuwa anakufa na alipogeuka hakumuona badala yake aliona sehemu ya maji ikiwa inafukuta.

“Huyu alikuwa kwenye mtumbwi ametangulia na Lugoye alikuwa na mtumbwi wake ghafla Shida akasikia kishindo puuuu!!! na sauti moja tu ya kilio ‘mayo nacha’ yaani mama nakufa alipogeuka hakumuona ndipo alipopiga kelele kuomba msaada” Makamba alieleza

Amesema wavuvi na wananchi wengine waliokuwa karibu walijitokeza kujaribu kutafuta lakini hawakubahatika kumpata bali waliukuta mtumbwi aliokuwa akiutumia ukiwa hatua chache kutoka eneo hilo..

Mazingira Fm ilimtafuta kijana aliyekuwa pamoja na Lugoye katika tukio hilo anayejulikana kwa jina la Shida amesema yeye akiwa ametangulia hatua kadhaa ghafla nyuma yake alisikia kishindo kama mtumbwi uliokuwa nyuma yake unapigwa kisha akasikia mwenziye anapiga kelele

Anasema kwa hiyo aligeuka kuona nini kimetokea lakini hakumuona mwenzake katika mtumbwi na badala yake aliona sehemu ya maji ikiwa na mvurugano hisia zikamtuma huenda inaweza kuwa mnyama kibogo au mamba hivyo alipata hofu na kupiga kasia kwa haraka kutoka eneo hilo na kwenda kutafuta msaada

Shukurani au Shida aliyekuwa na Lugoye

“Nilipiga kasia kwa kusogea mbali na eneo hilo huku nikipiga kelele na kuomba msaada kwa wenzetu na walipokuja tulirudi kwenye eneo hilo na kujaribu kumtafuta lakini hatukumpata ila kwenye mtumbwi wake tulikuta tochi, yeboyebo na panga vitu alivyokuwa navyo Lugoye” Shida alieleza.

Kufuatilia tukio hilo wananchi walikusanyika mida ya asubuhi na kuanza zoezi la utafutaji bila mafanikio na ilipofika saa sita mchana walisitisha zoezi la utafutaji na leo zoezi la utafutaji linaendelea tena kwa siku ya pili ikiwa upande wa familia tayari wameshaweka msiba wa ndugu yao.

By Edward Lucas