Loliondo FM

Ngorongoro yakubali Chanjo ya Uviko-19.

8 November 2021, 2:37 pm

Na EDWARD SHAO

Utoaji wa chanjo ya Uviko-19 wafikia asilimia 31 wilayani Ngorongoro tangu chanjo hiyo izinduliwe rasmi Agosti 3 2021 na mkuu wa wilaya Mh. Mwl Raymond Stephen Mwangwala.

Akizungumza katika kikao cha kujenga uelewa juu ya Ugonjwa huo na umuhimu wa chanjo kilichofanyika hii leo katika ukumbi wa mikutano ya halmashauri katibu tawala kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Bw. Lemuel Kristian Kileo wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, amewapongeza timu ya uendeshaji wa huduma za afya wilaya kwa namna wanavyoendelea na kusimamia zoezi zima la utoaji wa chanjo hiyo hadi kufikia asilimia 31, ambapo wilaya ilipokea mgao wa dozi 2,880 na kwa sasa chanjo hiyo inaendelea kutolewa katika vituo vya awali 15.

Ameongeza kuwa hivi karibuni wizara ya afya ilitoa muongozo kuhusu walengwa wa chanjo ya uviko-19 kuwa ni watu wote wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na makundi ya kipaumbele kwa lengo la kuchanja angalau asilimia 60 ya Watanzania wote, ameongeza kuwa makundi hayo ya kipaumbele yaliyoainishwa ni watumishi wa afya,wenye magonjwa sugu Kama kisukari,ugonjwa wa moyo,watu wenye umri kuanzia miaka 50,waongoza watalii,watu walio mipakani na tasisi za elimu ambapo chanjo hii inatolewa bila malipo.

Kwa upande wa washiriki wa kikao hicho ACP Fatuma Salum na Elias kalumbwa ambao ni miongoni mwa wahanga wa ugonjwa wa covid 19 wameeleza namna ambavyo ugonjwa huo ni hatari endapo utaupata ukiwa hujapata chanjo na kuahidi kwenda kutoa elimu kwa jamii ili wapate chanjo ya uviko-19 kwani ni salama na haina shida yoyote katika Afya

Kikao hicho kimewahusisha, wataalamu mbalimbali wa afya,Madiwani,viongozi wa ulinzi na Usalama,viongozi wa dini,mashirika yasiyo ya kiserikali,na viongozi wa mila.