Kitulo FM

Mvua yaleta maafa Makete, wananchi watakiwa kupanda miti kwa wingi

November 17, 2023, 7:46 pm

Diwani wa kata ya Iwawa Mh Fransic Chaula akitoa mkono wa pole kwa moja ya waathirika na mvua iliyosababisha nyumba kuezuliwa na upepo. Picha na Ombeni mgongolwa

Kutokana na Mamlaka ya Hali ya Hewa kutangaza mvua nyingi, wananchi wameaswa kupanda miti katika maeneo yao ili kuepukana na adha ya kuezuliwa nyumba zao.

Na mwandishi wetu.

Mkuu wa wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda ametoa pole kwa wananchi wa Dombwela walioharibiwa nyumba zao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, huku akitoa tahadhari kwa wananchi kupanda miti kwenye maeneo ya wazi ili kuzuia matatizo yanayojitokeza kupitia mvua.

Mhe. Sweda amesema hayo leo Novemba 17, 2023 wakati alipokwenda  kuwatembelea wananchi waliopata kadhia hiyo ya kuezuliwa kwa nyumba zao kutokana na mvua iliyonyesha tarehe 14 Novemba, 2023 wananchi hao ni Matrida Msigwa, Feidon Kyando, Ammy Sanga, Kasim Sanga na Joshua Mahenge.

Sauti ya DC Sweda
Baadhi ya viongozi wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Makete wakati wa kutoa pole kwa waathirika na mvua.

Mbunge wa jimbo la Makete Mh. Festo Sanga ametoa pole kwa wananchi waliopata dhoruba hiyo, huku akiwaasa kuchukua tahadhari mapema kama mamlaka ya hali ya hewa ilivyosema kutakuwa na mvua nyingi mwaka huu.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Makete Mh Festo Sanga

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Makete Mh Clement Ngailo amesema kuwa serikali inatambua uwepo wa wananchi waliokumbwa na shida hiyo ya kuezuliwa nyumba zao kuwa wapo pamoja nao kwa kipindi kigumu wanachopitia.

Sauti ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Mh Clement Ngailo
Moja ya nyumba iliyoezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali

Kwa upande wa diwani wa kata ya Iwawa Francis Chaula amesema wananchi wamejitaidi kama wanavyofanya maendeleo kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao kwa lengo la kuwafanya wapate hifadhi mpaka pale ambapo hatua zitakapochukuliwa huku akitoa shukrani kwa viongozi waliokuja kwa ajili ya kwenda kuwaona wananchi waliokumbana na shida hiyo.

Sauti ya diwani wa kata ya Iwawa Francis Chaula
Nyumba iliyoezuliwa na upepo mkali wakati wa mvua

Kwa upande wake, Diwani Viti Maalum kata ya Iwawa Mhe. Anifa F. Sanga amewashukuru madiwani wenzake Kwa upendo huo wa kuamua kuwashika mkono wahanga wa mvua, ambazo zimepelekea kuezuliwa kwa nyumba pamoja na baadhi ya kuta kudondoka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Dombuela, Mhe. Joseph Mbilinyi, amelishukuru Baraza la Madiwani kwa kuamua kuwatembelea na kuwashika mkono wahanga hao, ambao wamekuwa na wakati mgumu baada ya kutokea kwa janga hilo.

Hata hivyo waathirika wa mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali kuezua nyumba zao akiwemo mama Winnie wa Dombelwa wamewashukuru viongozi hao wakiongozwa na mkuu wa wilaya kwa kuwatembelea na kuwafariji.