Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka akiangalia mifuko ya Mchanga kwenye moja ya ghala la Mbolea
Kitulo FM

Waziri wa Kilimo aagiza Msola akamatwe

March 5, 2023, 2:51 pm

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameagiza kukamatwa na kuhojiwa Meneja Masoko wa Kampuni ya mbolea ya Minjingu Dkt. Mshindo Msola, msimamizi wa ghala la mbolea ya Minjingu mkoa wa Njombe na Meneja wa Kanda wa Nyanda za Juu Kusini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Michael Sanga kwa tuhuma za kukutwa na mifuko 776 ya mchanga katika ghala la kampuni ya mbolea ya Minjingu ambayo inadhaniwa huenda inatumika kuchakachua mbolea inayouzwa na kampuni hiyo.

Bashe amesema tukio hilo ni hujuma ambayo haivumiliki, ambapo atahakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua.

Ametoa agizo hilo baada ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na wale wa kamati ya siasa ya mkoa huo wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo Antony Mtaka kufika katika ghala hilo na kukuta shehena ya mifuko ya mchanga katikati ya mifuko ya mbolea ya Minjingu.