Wananchi wakosa huduma ya Umeme kwa zaidi ya mwezi sasa
Kitulo FM

Gharama za Maisha zapanda baada ya kukosekana huduma ya Umeme

March 5, 2023, 2:58 pm

Kutokana na mashine umba (Trasfoma) ya umeme kupata hitilafu katika kijiji cha Masisiwe wilayani Makete mkoani Njombe kumepelekea gharama za maisha kupanda kijijini hapo.

Wakizungumza kijijini hapo baada ya kufika na kujionea malalamiko hayo wananchi wameeleza kuwa baada ya kuepelekewa umeme huo wameutumia kwa kipindi kifupi na baadaye wamekosa huduma hiyo huku wakielezwa kuwa suala hilo lipo chini ya Mkandarasi wa REA.

Alfonce Sanga na Godfrey Sanga ni wananchi wa Masisiwe wamesema kwa sasa shughuli nyingi hazifanyiki kwasababu ya kukosa umeme.

Zephania Mtaita ni Mwenyekiti wa kijiji hicho amesema kuwa imefika hatua wananchi wanasaga Debe moja la Mahindi katika vijiji vya jirani vya Utweve na Tandala kata nyingine Na gharama inaweza kufikia mpaka shilingi elfu kumi na mbili (12,000) kwenda na kurudi.

Meneja wa Tanesco wilaya ya Makete ndugu Henriko Renatus amesema shida ya umeme imesabishwa na hitilafu ya mashine umba (Transfoma) na taarifa ya jambo hilo iko chini ya mkandarasi wa Wakala wa usambazaji wa umeme Vijijini (REA).

Kwa upande wake Meneja wa miradi ya REA upande wa mkoa wa Njombe Mhandisi Nickolas Lazaro amesema tayari amemwagiza msimamizi wake wilaya ya Makete ili kuifanyia uchunguzi Njia hiyo ya umeme ili kupatia ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Kuhusu ni lini umeme utawaka tena kijijini hapo, Mhandisi Lazaro amesema wananchi wawe watulivu kwani ni mategemeo yao kwamba ndani ya wiki hii huduma hiyo inaweza kurejea kama livyokuwa hapo awali.

Wananchi wakosa huduma ya Umeme kwa zaidi ya mwezi sasa