Kitulo FM

Wazazi Sababu Wanafunzi kufanya Vibaya Mitihani

January 25, 2023, 2:18 pm

Wazazi na walezi katika kijiji cha nyamande kilichopo kata ya kitandililo halmashauri ya mji wa Makambako wametajwa kuwa sababu ya wanafunzi hasa wa darasa la saba kufanya vibaya katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.

Wazazi hao wametajwa kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya mtihani wa mwisho na kuwatisha hali ambayo imesabibisha shule ya msingi nyamande kuwa ya mwisho kihalmashauri.

Kutokana na hali hiyo diwani wa kata ya kitandililo Imani Fute amelazimika kukaa na wazazi wa wanafunzi wa darasa la nne na la saba na kuagiza baraza la kata kuwachukulia hatua wale wote ambao wameshindwa kuwatimizia mahitaji ya msingi watoto wao.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamande Theresia Chengula amekiri kuwepo kwa tabia za wazazi kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mtihani wa mwisho na kueleza kuwa kwa sasa wamejipanga kuhakikisha shule hiyo inaingia kwenye shule kumi bora kihalmashauri.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Nyamande Elicado Mgohole amesema ataendelea kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wote ambao hawawajibiki katika nafasi zao hasa kuwahudumia watoto wao.

Kwa Upande Wao baadhi ya wazazi wamekiri kuwepo kwa tabia hiyo na kuiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao wanawashawishi watoto kufanya vibaya katika mtihani wa mwisho wa kuhitimu elimu ya msingi.